Chama cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA kimelitaka Jeshi la Polisi nchini kutoa taarifa rasmi juu ya matukio ya kuwakamata na kuwapekua viongozi wa kisiasa katika ngazi mbalimbali nyakati za usiku bila ya kuwepo na sababu zozote zenye misingi ya kisheria.
Hayo yameelezwa na taarifa iliyotolewa na Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa chama hicho, Tumaini Makene leo Aprili 25, 2018 na kusema jeshi hilo limeendelea kuwashikilia kinyume cha sheria kwa kuwanyima dhamana na kutowafikisha mahakamani
Aidha, Makene amesema baadhi ya maeneo ambayo hadi sasa viongozi wa CHADEMA wamekumbana na manyanyaso na ukiukwaji huo mkubwa wa haki za binadamu na sheria za nchi unaofanywa na polisi ni Dar es Salaam, Geita, Pwani, Njombe, Iringa, Arusha, Morogoro na Tanga.
"Tunapinga na kulaani vikali vitendo hivyo vya ukiukwaji wa haki za binadamu na sheria za nchi yetu na tunasisitiza kuwa havikubaliki katika jamii yeyote inayozingatia kuwa haki ni msingi muhimu wa amani na utulivu wa kweli.Tunatumia nafasi hii kulikumbusha Jeshi la Polisi nchini kuwa lina wajibu wa kutekeleza majukumu yake kwa kuzingatia Katiba, Sheria za Nchi na weledi unaokubalika", amesema Makene.
Kwa upande mwingine, Makene amesema chama chake kimetoa maagizo kwa wanasheria wake kupitia Kurugenzi ya Katiba na Sheria, kufuatilia suala hilo kwa ukaribu na kuchukua hatua za haraka za kisheria.
Post A Comment: