Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimefanya mkutano na waandishi wa habari na kudai kwamba ukiachilia mbali kiwango za zaidi ya shilingi trilioni 1.5 ambazo zilidaiwa na Zitto Kabwe kwamba hazifahamiki zimekwenda wapi katika ripoti ya CAG, kuna kiwango kingine kikubwa cha fedha pia kimetumika hovyo.

Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Uenezi wa Chadema, John Mrema, leo Aprili 18, 2018 katika makao makuu ya Chama hicho, Kinondoni Dar, na kudai kuwa fedha nyingine zilizopotea ni za kwenye mashirika ya umma yakiwemo ya mifuko ya hifadhi za jamii, ununuzi wa ndege na Shirika la Ndege kwa ujumla. Amedai chama chao kitatoa ufafanuzi wa kifungu kwa kifungu kuhusu ripoti hiyo ya CAG.

“Baada ya sakata hili la trilioni 1.5, kuna wanasiasa hasa wa ccm wanataka kubadilisha mjadala huu na kuanza kusema eti Chadema kuna ufisadi,” alisema John Mrema.

Hata hivyo, Serikali kupitia kwa Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Ashatu Kijaji amesema hakuna fedha taslimu kiasi cha shilingi trilioni 1.51 iliyopotea au kutumika kwa matumizi ambayo hayakuidhinishwa na Bunge.

Pia, Rais Dkt. John Pombe Magufuli amesema kuwa katika ripoti ambayo alipokea kutoka kwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Prof. Mussa Assad haikuonyesha upotevu wa fedha hizo na kueleza endapo kungebainika kitu kama hicho, basi aliyehusika angechukua hatua kali siku hiyo hiyo.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: