JANUARY Makamba, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais anayeshughulikia Muungano na Mazingira ametoa madai mazito kwa chama chake, kuwa Chama cha Mapinduzi (CCM) kimemtelekeza baba yake Mzee Yusuph Makamba akiwa mgonjwa.

Makamba ameandika ujumbe huo katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Facebook, akielezea hali ya baba yake kiafya na kusema pamoja na kupitia hali hiyo lakini CCM hakimpi stahiki zake kama mstaafu wa chama hicho.

Mzee Makamba ameshika nafasi mbalimbali katika chama lakini kikubwa zaidi ni kuwa Katibu Mkuu cha chama hicho, pamoja na nafasi mbalimbali serikalini ikiwemo Mkuu wa mikoa mbalimbali ukiwemo Dar es Salaam.

Katika taarifa hiyo ya January pia imeeleza tuhuma za wanasiasa aliowalea Mzee Makamba ambao mmoja wao kwa sasa anasema maneno mabaya dhidi ya mzee huyo.

Soma andiko la January hapa chini:

Majuzi nilienda kumjulia hali Mzee Makamba ambaye anaumwa. Mazungumzo yake yalihusu watoto wake aliowalea kisiasa, ambapo mmoja wapo, pamoja na kumhifadhi na kumfariji wakati kasahaulika, sasa anasema maneno mabaya dhidi yake.

Tukazungumzia subira na uvumilivu kwenye siasa. Akaamua kunipa kisa kifuatacho:

Mwaka 1980, baada ya kutoka vitani, alipangwa kuwa Katibu Msaidizi wa CCM Dodoma. Mwaka 1982, wakati wa kuadhimisha miaka 5 ya kuzaliwa kwa CCM kimkoa kule Mvumi, alitumwa mnadani Mwitikira kununua kitoweo (ng’ombe na mbuzi) kwa ajili ya sherehe.

Baada ya muda, akiwa kahamishiwa Monduli, akapewa barua ya kusimamishwa utumishi na uongozi (u-NEC) wa CCM kwa tuhuma kwamba wale ng’ombe na mbuzi wa sherehe aliwaswaga kwetu Bumbuli badala ya kuwapeleka Mvumi.

Tukafungasha mizigo na kurudi kijijini. Wakati Mzee anaendelea kutafuta maisha kijijini alikuwa anaandika barua kila siku Ikulu kwa Mwalimu Nyerere kueleza kwamba ameonewa. Baada ya barua kadhaa, Mwalimu akaagiza aitwe kwenye kikao cha Kamati Kuu Chamwino Dodoma. Mzee aliwasili Dodoma akiwa kachoka sana, amebeba makabrasha yake kwenye mfuko wa rambo.Makambazzz

Kikao kilipoanza, Mwalimu akampa nafasi Mzee Makamba ya kujieleza. Mzee akaanza kwa kusema ana hoja nyingi kuonyesha kaonewa lakini angependa kuanza na swali dogo: “Kwenye ile sherehe, Ndugu Moses Nnauye alikuwa mgeni rasmi na alikula ubwabwa. Ndugu Mwenyekiti, naomba aulizwe iwapo ubwabwa ule aliokula ulikuwa na nyama au la.” Mwalimu akamgeukia Nnauye na kumuuliza “Moses, Yusuf anauliza iwapo ubwabwa uliokula ulikuwa na nyama.” Nnauye akasimama na kujibu “Mwenyekiti, ubwabwa ulikuwa na nyama.” Mzee akaendelea “iwapo niliswaga ng’ombe kijijini kwetu, hiyo nyama kwenye ubwabwa ilitoka wapi?” Mwalimu akawageukia watendaji waliotengeneza mashtaka ili watoe majibu. Kukawa hakuna jibu. Baada ya Mzee kujieleza tena kwa kifupi ikadhihirika wazi kabisa kwamba kulikuwa na uonevu mkubwa. Akarudishwa kazini.

Wakati Mzee ananipa kisa hiki, alikuwa anajichoma sindano ya “insulin” kudhibiti kisukari, huku akigusa jicho lake moja ambalo linakaribia kuwa pofu. Amegoma kabisa kutibu jicho akisema “hata likiacha kuona, sio tatizo kabisa; limeshaona mengi humu duniani”

Kwa sasa Mzee hali yake kiafya sio nzuri chama cha mapinduzi hakimpi stahiki zake kama mstaafu.

Share To:

msumbanews

Post A Comment: