Benki ya Dunia (WB) imekubali kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika kukabiliana na athari za mafuriko zinazosababishwa na mvua kubwa zinazonyesha kila mwaka katika Jiji la Dar es Salaam na kuleta madhara makubwa hususan katika eneo la Jangwani jijini humo.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) wakati akizungumza na ujumbe wa Benki ya Dunia ulioongozwa na Mkurugenzi wa Benki hiyo kwa nchi za Tanzania, Somalia, Burundi na Malawi Bi. Bella Bird, katika mikutano ya kipupwe inayoendelea mjini Washington DC.
Dkt. Mpango amesema kuwa Benki ya Dunia imekubali kusaidia kukabiliana na mafuriko katika bonde la mto Msimbazi hasa katika eneo la kutoka Magomeni Mapipa kwenda Faya na tayari Benki hiyo imeanza zoezi la kutafiti eneo la Jangwani ili kuweza kuangalia namna nzuri ya kugharamia uboreshaji wa mifereji katika bonde la mto Msimbazi ili kumaliza kero hiyo kwa wananchi wa Dar es Salaam.
“Tumewaeleza Benki ya Dunia changamoto hii ambayo imekuwa inajirudia kila mara na kusababisha upotevu wa maisha ya watu, kusababisha kufungwa kwa barabara, watu kushindwa kwenda kazini na wanafunzi kushindwa kwenda shule, hivyo wameonesha nia ya kumaliza kero hii kwa wananchi,” alisema Dkt. Mpango.
Amesema kuwa baada ya timu ya Benki ya Dunia kumaliza kufanya kazi yao kwa kushirikiana na Manispaa ya jiji la Dar es Salaam, Serikali inaamini njia ya kudumu itapatikana na kuondokana na tatizo hilo la mafuriko ya mara kwa mara katika eneo la Jangwani.
Post A Comment: