Kwanza tuwekane sawa… Kwa daraja la Neymar Jr mpaka anafikia maamuzi fulani kwenye maisha yake ya soka, Kuna kundi kubwa la binadamu wenye akili nyingi limechangia mawazo… Kuanzia kwenye kulinda kipaji chake, jina lake, biashara na kesho yake…
Tukisoma waraka wake alioweka kwenye ukarasa wa instagram baada ya uhamisho wake kwenda PSG alijaribu kukwepa kuwa Baba yake hakuhusika hata kidogo. Mwenyewe anakiri kuwa ndiye aliyemlazimisha baba yake katika maamuzi haya…
Nimeiona akili ya Neymar Jr niliposoma ile nukuu ya Marehemu Yohan Cruyjf…
Alisema hivi “Epukeni kutengeneza zizi moja na kuweka mafahari wawili”.

Ni wazi kuwa Neymar ni mchezaji mkubwa wa kariba ya Lionel Messi ikiwa amewahi kushindana nae kwenye tuzo kubwa za Ballon d’Or.. Usinielewe vibaya.. Nimezungumzia usawa wa kiushindani na sio suala la kipaji cha mtu na mafanikio yake
Neymar alibet sijui kama mkeka wake utatki.
Kwanza ametazama kuwa Barca inaenda kupotea imeachana na utamaduni wake na imeanza kuingia Masokoni. Ubora wao kimwili uko karibu na jeneza kuliko mikono ya madaktari… Wazo hili huenda lipo sahihi kwake. Wakati Robinho anakwenda Real Madrid dunia ilijua tuzo ya Ballon d’Or aliyoshikilia Ricardo Kaka (wa mwisho kutoka Brazil) Robinho nae atatua nayo pae Sao Vicente mji aliozaliwa.
Romario alitwaa tuzo ya BDO mwaka 1994. Kisha baadae Ronaldo mwaka 1996 na 1997, kisha akaongeza ya tatu mwaka 2002. Rivaldo nae hakufanya makosa 1999, Ronaldinho akaipokonya mwaka 2004 na 2005, mwisho wa furaha ya wa Brazili ni Kaka mnamo mwaka 2007.
Je yeye ni wa kwanza
Hapo awali nimemgusia kidogo Robinho. Mnamo mwaka 1999 Pele alisimama kama kidume na kusema kuwa Robinho akiwa na miaka 15 tu kuwa ndiye mrithi halali wa ufalme wake. Robinho alijunga Real Madrid.

Maisha yake Madrid hayakuwa Mabaya Maana Msimu wake wa kwanza alimaliza na magoli 14 kwenye michezo 37 akiwa na msimu bora kabisa. Mnamo mwaka 2006 Fabio Capello hakumtumia sana, licha ya kufunga magoli 11 na kutengeneza magoli 8. Katika maisha yake Madrid yeye alikuwa mfungaji bora namba tatu mwenye magoli mengi akiwa nyuma ya Raul Gonzalez na Ruud Van Nestelrooy . Pia alikuwa na asisti nyingi nyuma ya Guti. Kama haitoshi yeye na Iker Casilasi ndio wachezaji pekee waliongia Orodha ya wachezaji 10 waliogombania BDO.
Lakini aliposikia ujio wa Cristiano Ronaldo aligoma kusaini mkataba mpya kwa kile alichodai kuwa atakuwa nyuma ya kivuli cha Ronaldo aliyetwaa tuzo ya BDO akiwa na Man utd. Uoga ule wa Robinho ulimfanya akimbilie fedha za Mabwenyenye wakiarabu Wa Man city akidai kuwa anataka kushindana akiwa zizi tofauti na Ronaldo.
Kwanini neymar ameamua haya..
Wakati Pirlo anaenda Juventus aligundua kuwa Clarence Seerdof, Philippo Inzzagh, Yepes, Mark Van Bormell, na wengine wengi umri umeenda.. Ufalme wao ulikuwa jirani na mauti kando ya kaburi. Alichokifanya Neymar kupigana na Semedo hata Andrea Pirlo alikifanya kwa Mark Van bomell kwa baada ya kumpiga na kiwiko kwenye mazoezi.
Kabla ya kumuwaza huyu fundi wa Kibrazil mwenye miguu yenye nta iliyofunga ndoa ya Kikristu na mpira… Jaribu kuangalia umri wa Gerrard Pique, Lionel Messi, Andrea Iniesta na Suarez? Ni dhahiri bibi harusi ataolewa na ujauzito, je mtoto atakuwa wa nani?
Ricardo Kaka alipoona Ac Milan inapotea, naye hakususua kupokea kile kilichotoka kwenye mfuko wa Perez… Uchizi siyo kupokea ila kutopokea angekuwa mwendawazimu kamili…
Neymar aligundua kizazi cha La Masia ndio siri ya mafanikio ya Barcelona lakini inaonekana kama wanaotoka La Masia siku hizi wana vyeti feki hivyo hawapati nafasi Barcelona kubwa.
Pengo la Puyol mpaka sasa halijazibika…na hicho ndicho alichokicha Maldin 2010 baada kustaafu. Ajabu ni kwamba Masimillano allgeri alimkimbilia Bwana Mdogo Zlatan bila kuangalia mbadala wa Maldin ni nani. Kule katalunya nako Ndicho kilichopo kwenye pengo la Xav. Leo hii wamekuja Rakitic na Gomes, unadhan kuondoka kwa Kaka na Seerdoff kungeicha Ac milan salama?
Kama sio je unategemea mapengo haya ya Barcelona yatazibwa na meno bandia? Yaani Hata kivuli cha Alves holaaa… bado ule unyunyu wake mashambulizi kutoka mbavu za kiumeni kulia haupo Gomes anakimbia kama ametoka jando la kimasai. Iniesta huyooo anasepaa umri hauna urafiki na mapafu, akili yake nayo iniashtak miguu yake kwa kutokufanua kile kinaishtaki.
Binafsi kwangu mimi Messi ni kama anaelekea kuvunja ndoa ya kwenye ubora wake muda sio mrefuu. Hilo lipo wazi. Mpaka sasa anaendelea kutawala kwa nguvu ya dola na siyo matakwa ya sanduku la wapiga kura….
Kwahiyo?
Neymar hapo aligundua anahitaji miaka miwili mpaka mitatu tu magazeti yataanza kuita Messi flop na Ronaldo veterani.. Wakati huo atakuwa ana umri wa miaka 27, ni kipindi na nyakati muafaka kabisa wa kiwango cha mchezaji bora wa dunia. Amegundua PSG ndiyo sehemu salama kwake kwa miaka ijayo maana anaamini kwenda kwake pale kutawavuta na wengine.
Mpaka hapo washindani wake ni Hazard, Griezman, Delle Ali, Pogba na Dybala kama siyo Mbappe..Hana cha kupoteza hapo… labda Sepp Blatter arudi tena kuwa rais wa Fifa hiyo tuzo ampe Messi kama ile ya 2010 ambayo hata mtoto wangu aliyekuwa tumboni wakati huo aliamini Xavi, Iniesta na Sneijder mmoja wao alistahili. Hata ile ya 2014 mikono salama ya mlinda milingoti mitatu ya Ujerumani na Bayern alistahili. Lakini Fifa ya Blatter ikapeleka virungu kwa wapiga kura bila kujali takwimu.
Neymar anaamini katika kipindi cha miaka miwili ijayo atasifiwa kwa kuwa mbeba timu ya PSG na anafahamu fika kuwa La Liga inabebwa na Messi na Ronaldo. Anataka na yeye asemwe Ligue One ni ya Neymar Jr tu… Anajua hata Barcelona ikibeba kombe la Fly Emirates sifa ni kwa Messi… sasa kwanini asiende mahala ambako ana uhakika wa vikombe ambavyo magazeti ya le Quipe yatapambwa na picha zake?
Kama Barcelona itashindwa kuziba pengo la Xavi, Puyol na Iniesta msishangae kuona muda sio mrefu Messi naye huyoo kasepa…
Neymar Jr ameona mifuko miwili…
Mfuko wa lawama za Barcelona mbovu atakayoachiwa na Messi… au mfuko wa Billion 40 kwa mwaka kutoka kwenye vikoi na kanzu za Kiarabu..
Barca nao vipi walikuwa sahihi kumwachia Neymar?
Kwa akili ya kawaida hata ungekuwa wewe Raisi wa Barcelona huwezi kataa kitita cha milion 222 ikiwa bingwa wa UEFA fainali anakabidhiwa E15 tu. Je huyo Neymar unayetaka akupe UEFA utahitaji UEFA ngapi ili ifikie hicho kiasi?
Hata akibaki akatwaa BDO 10 je zitaipa timu milion 222? Tena kwa dunia hii Coutinho anauzwa 100, Na mbappe 120 haikuwa rahisi kukataa kiasi kile cha pesa ambacho hata Neymar angeuza jezi vipi kisingefika.
Sawa walipokea kiasi hicho na timu imeyumba wewe huoni kama walipolea rambirambi za kujizika? Kumpoteza Neymar kwa Barcelona ni pengo kubwa mno. Barca kwa sasa inafanya vizuri kwa sababu tu ya mgongo wa Messi. Muda sio mrefu tutaongea mengine
Share To:

msumbanews

Post A Comment: