Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro Clifford Tandari ameishauri Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kusomesha vijana wengi katika fani ya ufundi ili kupata wataalamu watakaofanya kazi katika viwanda ili kuendana na sera ya serikali ya awamu ya Tano ya kuwa na uchumi wa Kati na wa viwanda ifikapo mwaka 2015.
Tandari amesema hayo Mkoani Morogoro wakati akifungua Mkutano wa 25 wa Baraza la wafanyakazi wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia na kusisitiza kuwa Serikali inayoongozwa na Rais John Pombe Magufuli imeweka misingi imara itakayowezesha kila Mtanzania kupata Elimu bora na yenye tija kwa Taifa ili kufikia malengo ya Taifa.
Akizungumza na baraza hilo la Wafanyakazi Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dk. Leonard Akwilapo amesema kufanyika kwa baraza hilo ni matokeo ya utekelezaji wa Sera ya kuwashirikisha wafanyakazi katika uongozi wa pamoja mahali pa kazi na kuwa mkutano huo pia utapitia na kujadili utekelezaji wa bajeti ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia mwaka 2017/18 na mwelekeo wa bajeti ya mwaka 2018/19.
kwa upande wake Katibu wa Baraza la Wafanyakazi wa Wizara hiyo Gerald Mweli amesema Baraza hilo ndio chombo cha juu kabisa cha sheria ya majadiliano kazini kinachojumuisha wafanyakazi wote kujadiliana kwa pamoja mafanikio, changamoto na kuweka mipango ya namna ya kutatua changamoto zinazowakabili.
Mkutano huo wa siku mbili ulioanza leo utakamalizika kesho ukiwa na kauli mbiu inayosema “Elimu Jumuishi, Sayansi na Teknolojia ni Msingi wa maendeleo Endelevu ya Uchumi wa Viwanda Tanzania”.
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano Serikalini,
WIZARA YA ELIMU, SAYASNI NA TEKNOLOJIA.
23/04/2018
Post A Comment: