Na George Mganga
Ligi Kuu Bara imeendelea Jumapili ya leo kwa mechi tatu kupigwa viwanja tofauti huku mchezo mmoja kati ya Azam FC dhidi ya Njombe Mji ukisubiriwa usiku huu.
Lipuli FC ilikuwa ikiikaribisha Singida United katika Uwanja wa Samora mjini Iringa na kufanikiwa kuibuka na ushindi wa bao 1-0. Bao hilo limefungwa na Malimi Busungu dakika ya 17.
Mechi nyingine iliyokuwa inasubiriwa kwa hamu mkoani Shinyanga ilikuwa ni dabi kati ya Mwadui FC dhidi ya Stand United katika mchezo ambao umemalizika kwa wenyeji Mwadui kukubali kichapo cha mabao 3-1 ikiwa Uwanja wake wa nyumbani, Mwadui Complex.
Mabao ya Stand United yametiwa kimiani na Tariq Seif (51'), Seleman Ndikumana (61') na Sixtus Sabilo (85'). Mwadui FC walejipatia bao lao mnamo dakika ya 76 kupitia kwa Abdallah Seseme.
Mbao FC nayo ilikuwa mwenyeji dhidi ya Majimaji FC kwenye Uwanja wa CCM Kirumba Mwanza ambapo mtanange huo umeenda sare ya mabao 2-2. Mbao wamepata mabao hayo kupitia kwa Boniface Maganga katika dakika za 60 na 62 huku Marcel Kaheza akiifungia Majimaji kwenye dakika za 81 na 90.
Mechi ambayo inaendelea hivi sasa ni kati ya Azam FC iliyo Uwanja wa Complex dhidi ya Njombe Mji FC.
Post A Comment: