KLABU ya Manchester United iliyomo katika Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) jana ilitangaza kuachana na mshambuliaji wake, raia wa Sweden, Zlatan Ibrahimovic.
Mchezaji huyo, katika kipindi cha miezi 12, amekuwa akisakamwa na majeraha mbalimbali yakiwemo maumivu ya goti aliyoyapata mwezi Agosti mwaka jana, hali iliyomweka pabaya katika klabu hiyo ya Mashetani Wekundu.

Licha ya kuisaidia klabu hiyo kushinda katika Ligi ya Europa, kurejea kwake katika klabu hiyo kumethibitika kuwa jambo gumu. Hili limejionyesha katika taarifa iliyotolewa na klabu hiyo ikimshukuru mchezaji huyo kwa mchango wake.
“Manchester United inathibitisha kwamba imekubali kuvunja mkataba na Zlatan Ibrahimovic mara moja. Kila mtu kwenye klabu ni dhahiri atamshukuru Zlatan kwa mchango wake tangu afike hapo na kumtakia kila jema katika maisha yake ya baadaye,” ilisema taarifa hiyo.

Naye Zlatan aliposti ujumbe kwenye Instagram yake baada ya taarifa hiyo ambapo alisema: “Mambo makubwa huja na kufikia mwisho na ni wakati wa kuondoka baada ya misimu miwili ya kufurahisha na Manchester United. Asante ziiendee klabu, mashabiki, timu, kocha, wafanyakazi na kila mtu ambaye alishiriki name katika sehemu hii ya historia yangu.”
Zlatan (36) ni mchezaji mahiri aliyechezea klabu kadhaa za ligi kuu barani Ulaya zikiwemo Paris Saint-Germain ya Ufaransa, Juventus, Inter na AC Milan za Italia, Barcelona ya Hispania na Ajax ya Amsterdam, Uholanzi.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: