Na Ferdinand Shayo, Arusha.
Waziri wa Tamisemi Suleman Jafo amesema kuwa serikali haitasita kuwachukulia hatua watumishi Wazembe katika vituo vya afya ambao hawatoi huduma bora kwa wananchi licha ya maboresho ya vituo vya afya yanayofanyika katika vituo vingi vya serikali kwa kujenga majengo ,dawa na vifaa tiba vya kisasa.
Jafo amesema hayo wakati akikagua ukarabati na ujenzi wa kituo cha afya cha Usa river kilichopo Wilaya ya Meru mkoani Arusha ambapo ameitaka Halmashauri hiyo kuharakisha ujenzi wa chumba cha upasuaji pamoja na wodi ya mama na mtoto ili wananchi waweze kupata huduma bora zilizoboreshwa na serikali.
Aidha amepongeza kasi ya ujenzi wa kituo hicho na kazi nzuri inayoendelea ,ukarabati unaokwenda sambamba na ukarabati na ujenzi wa vituo vingine zaidi ya 200 ambavyo serikali imelenga kuhakikisha kuwa watanzania wanasogezewa huduma za afya karibu na maeneo wanayoishi.
Jafo amewataka Watumishi wa Afya kufanya kazi kwa bidii na kutozembea katika utoaji wa huduma za Afya kwani Wizara yake haitasita kuwachukulia hatua Watumishi ambao ni wazembe.
Mwenyekiti wa Kamati ya Ukarabati na Ujenzi wa Kituo hicho John Molel amesema kuwa halmasahauri ya Wilaya ya Meru ilipokea kiasi cha shilingi milioni 500 ambazo zitatumika kukarabati na kujenga chumba cha upasuaji,wodi ya kinamama wajawazito pamoja na chumba cha kuhifadhia maiti.
Kwa Upande wao Wananchi wa Kata ya Usariver Emmanuel Kaaya na Lilian Katabali wamepongeza serikali kwa ukarabati unaondelea ambao utasaidia katika kuboresha huduma za afya kwani kipindi cha nyuma walisafiri umbali mrefu na kwenda kutibiwa katika hospitali ya Patandi .
Post A Comment: