WAZIRI wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, amewataka wakurugenzi wa halmashauri nchini kufikria namna ya kuogeza fedha za mikopo kwa ajili ya makundi ya wanawake na vijana.
Mwalimu Ummy alisema jana kuwa fedha zinazotolewa kwa makundi hayo kutoka vyanzo vya halmashauri ni kidogo na haziendani na uhalisia.
Alisema kwamba haiwezekani kikundi cha watu 15 wakakopeshwa shilingi 300,000 halafu ukategemea watapiga hatua.
Alitoa wito huo alipokuwa akihutubia katika sherehe za maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani kwenye uwanja wa Nelson Mandela mjini Sumbawanga, akiwa mgeni rasmi.
‘’Naagiza wakurugenzi wote nchini kutazama upya suala la mikopo ya wanawake na vijana inayotoka katika asilimia tano ya mapato ya halmashauri kuwakopesha mikopo itakayowasaidia kufanya shughuli na kupata faida,” alisema na kuongeza:
“Kwa sababu utakuta kikundi cha watu 15 wanapewa shilingi 300,000, fedha ambazo hazitoshi, walau ziwe hata shilingi milioni kumi kwa kikundi walau wanaweza kuzizalisha.”
Pia aliitaka jamii kubadili mtazamo wa kufikiria kuwapelekea misaada ya chakula na nguo watoto yatima na wanaoishi katika mazingira magumu, badala yake waanze kuwalipia huduma ya afya kupitia Toto Afya Kadi kwani miongoni mwa changamoto zinazowakabili watoto hao, ni pamoja na huduma za afya.
Naye Mbunge wa Sumbawanga Mjini, Aesh Hilary, alimuomba waziri huyo magari ya kubebea wagonjwa ambapo wanawake hususan kwa ajili ya wajawazito ambao wanahitaji huduma za dharura kwa kuwa mkoa huo wa Rukwa una changamoto ya upungufu wa magari hayo.
Baada ya kulisikia ombi hilo, Waziri Ummy aliahidi kutoa magari mawili ya kubebea wagonjwa ambapo moja litakuwa maalum kwa Hospitali ya Rufani ya Sumbawanga na lingine aliagiza kitafutwe kituo kilichopo mbali na mjini ndicho kipatiwe gari hilo.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Kalambo, Julieth Binyura, alimshukuru Ummy kwa kukubali kufika mkoani Rukwa na kusherekea na wanawake wa mkoa huo, akisema amewapa hamasa na kuwasaidia kutatua changamoto nyingi ambazo zitawafanya kuongeza ari katika utendaji kazi.
Post A Comment: