Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Harrison Mwakyembe amesema msanii Diamond anafaa kuwa balozi wa maadili kutokana na ushawishi alionao kwa sasa.
Waziri Mwakyembe amesema hayo baada ya kikao kilichowakutanisha watu wa Wizara hiyo, kutoka Baraza la Sanaa Taifa (BASATA) na menejiment ya msanii huyo ambapo walijadili mvutano uliojitokeza mara baada ya nyimbo mbili za Diamond kufungiwa.
“Ndio balozi wetu, balozi wa maadili pia, kwa sababu Diamond utake usitake yeye ni balozi wa Tanzania kwa kila kitu na safari hii tumemuomba hata maadili awe balozi wetu, kwa sababu watu wengi wanamfuta Diamond, yeye ni Super Star na tunajivunia Watanzania,” amesema.
Pia Waziri Dkt. Mwakyembe amesema maamuzi ya kuzifungia baadhi ya nyimbo yanafanywa kwa mujibu wa sheria na si kwa utashi binafsi wa kiongozi wa wizara, hivyo ieleweke kwamba hatua zilizochukuliwa na Naibu Waziri Shonza hivi karibuni zilikuwa za Wizara kwa mujibu wa sheria za nchi.
“Nawaagiza watendaji wa Wizara na Taasisi zake ikiwemo BASATA, Bodi ya Filamu na TCRA, kuweka madaraja ya kazi zetu za sanaa, kuna kazi za sanaa ambazo kuonekana ni kuanzia saa sita hadi saa 12 asubuhi na hii inafanyika nchi nyingi ndio maana nimesema wakae na wenzetu,” ameongeza.
Kwa upande wake Naibu Waziri, Juliana Shonza alisema suala la kulinda maadili ni endelevu na wakati umefika sasa kwa Bodi ya Filamu na TCRA kukamilisha zoezi la kuoanisha kanuni za madaraja ya kazi za sanaa ili kazi zinazofaa kuonekana na watu wazima zianze kuangaliwa saa sita usiku hadi saa 12 asubuhi.
Naye Diamond alisema, “Nitashirikiana kwa karibu na Naibu Waziri Shonza na uongozi mzima wa wizara katika kusimamia maadili ya kazi za sanaa na kuwa mfano bora wa wasanii nchini katika kulinda utamaduni wa mtanzania”.
Post A Comment: