Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo, Dkt. Harrison Mwakyembe pamoja na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Selemani Jafo wanatarajia kutoa maagizo mazito kwa Maafisa Mawasiliano wa Serikali katika mkutano wao wa mwaka unaofanyika leo Machi 12 hadi 16 mwaka huu Jijini Arusha.
Hayo yameelezwa na Mkurugenzi wa Idara ya Habari (MAELEZO) na Msemaji Mkuu wa Serikali Dkt. Hassan Abbasi mapema jana Jijini Arusha wakati wa ziara yake ya kutembelea vyombo vya habari mkoani humo.
“Maafisa Mawasiliano ambao pia wanatambulika kama Maafisa Habari ndio injini ya Serikali katika kuisemea na kutangaza shughuli mbalimbali zinazofanywa na Serikali ndani ya Taasisi na Idara za Serikali, Halmashauri, Miji, Majiji na Mikoa. Kila Afisa Habari anatakiwa kuwa na habari za eneo lake na kulifahamu vizuri,” alisema Dkt. Abbasi.
Hivyo basi katika kuhakikisha Maafisa hao wanafanya vizuri katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku mkutano mkuu wa mwaka huu utahudhuriwa na mawaziri wawili, Dkt. Harrison Mwakyembe ambaye atafungua mkutano huo na Selemani Jafo ambaye atafunga mkutano hao.
Aidha, Mawaziri hao watatoa maagizo mbalimbali juu ya namna Maafisa hao wanavyotakiwa kutoa taarifa za utekelezaji wa miradi na ahadi za viongozi kwa wananchi pamoja na kuwaeleza Wananchi namna Serikali inavyofanya kazi ili Wananchi wawe na uelewa na kujua kinachoendelea.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama cha Maafisa Mawasiliano Serikalini (TAGCO) Pascal Shelutete amesema mkutano wa mwaka huu unatarajiwa kuhudhuriwa na Maafisa Mawasiliano 300 kutoka Taasisi na Idara za Serikali, Halmashauri, Miji, Majiji na Mikoa yote Tanzania.
Mkutano Mkuu wa mwaka wa Maafisa Mawasiliano Serikalini unafanyika kila mwaka, ambapo kwa mwaka huu unafanyika kwa mara ya 14 ambapo lengo la mkutano ni kuwajengea uwezo Maafisa hao katika utekelezaji wa shughuli zao za kila siku.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: