Wananchi wanaotumia barabara ya Mianzini - Timbolo iliyotengenezwa kwa kiwango cha lami wamekiri kuanza kuona maendleo nyumbani kwa kuona manufaa ya barabara ya lami ingawa imetengenezwa kwa umbali mfupi ukilinganisha na urefu wa barabara hiyo.
Wakizungumza na mwandishi wetu wakazi wa Mianzini eneo la kwa Loning'o wamethibitisha kuridhishwa na ujenzi wa barabara hiyo na kudai kuwa tayari wameanza kuona mwanga wa maendeleo katika eneo lao.
Wamesema kuwa uwepo wa lami katika barabara hiyo ni neema kwao kwani wameisubiri tangu kuzaliwa kwao na kuongeza kuwa barabara hiyo imerahisisha usafiri kwa wakazi na wafanyabiashara wanaosafirisha mazao kutoka maeneo ya mlimani na kuyaleta mjini.
Hata hivyo wakazi hao wameiomba serikali kuongeza umbali wa ujenzi wa barabara hiyo kwa kiwango cha lami ifike mwisho na kuifanya barabara yote kuwa ni ya kiwango cha lami.
John Loshilu mkazi wa Mianzini amethibitisha kupata neema hiyo ya barabara kwa kusema kuwa wamenza kuona maendeleo katika eneo lao ambayo hayajawahi kutokea tangu kupatikana kwa uhuru wa Tanganyika.
" Awamu hii ya tano tumeanza kuyaona maendeleo, lami tulikuwa tunaiona mjini leo imefika katika eneo letu, kwa kweli hata kama haijafika mwisho lakini ni bora kuliko lile vumbi lilokuwa linatimka kwenye hii barabara" amesema Loshilu.
Barabara ya Mianzini - Timbolo yenye urefu wa takribani Kilomita 9 imejengwa kwa kiwango cha lami urefu wa Mita 800 kwa gharama ya shilingi milioni 408 fedha za ambazo hutolewa na serikali kama ruzuku ya barabara.
Naye meneja wa TARURA Mhandisi Kilusu Teteana amesema kuwa mpaka sasa wamemaliza hatua ya kwanza ya kutengeneza Mita 800 za barabara hiyo na kuongeza kuwa wataendelea kutengeneza barabara hiyo na kuikamilisha kadiri fedha zitavyopatikana.
Hata hivyo mhandisi Kilusu amewataka wananchi hao kuitunza barabara hiyo kwa kuacha tabia ya kuelekeza mifereji ya maji kwenye barabara pamoja na kuendelea kutunza hifadhi za barabara.
Post A Comment: