Kifo cha kutatanisha cha kijana anayejishughulisha na uuzaji wa machungwa jijini Mbeya, kimeibua vurugu kubwa za vijana wenzake kutokana na kuhusishwa na Jeshi la Polisi.
Kijana huyo aliyefahamika kwa jina la Allen Mapunda (20), alifariki dunia, siku moja baada ya kukamatwa na kukaa mahabusu kisha kupelekwa hospitali.
Alifia hospitali alikopelekwa kupatiwa matibabu ya majereha baada ya kukamatwa kwa tuhuma za uhalifu ambazo hazijawekwa wazi.
Mapunda alifariki dunia katika Hospitali ya Rufani ya Kanda ya Mbeya, baada ya kukaa kituo cha polisi kwa siku moja.
Inadaiwa kuwa kijana huyo mkazi wa Mtaa wa Iyela II anayefanya shughuli zake za ujasiriamali katika Soko la Sido jijini Mbeya, kabla ya mauti kumkuta alikamatwa Machi 24, mwaka huu majira ya saa nne usiku katika eneo la kucheza ‘pool’ Mtaa wa Maendeleo na kumpeleka hadi Kituo Kikuu cha Polisi.
Inadaiwa Mapunda alikuwa na vijana wenzake wakicheza mchezo huo na baada ya kuwaona polisi aliwaambia wenzake wakimbie, lakini wote walitiwa mbaroni.
Habari zaidi zinaeleza kuwa Mapunda alikaa kwa siku moja na kesho yake alidhaminiwa na ndugu ambao waliamua kumpeleka hospitali kwa ajili ya matibabu kutokana na majeraha aliyoyapata.
Kwa mujibu wa mama yake mlezi, Alice Mapunda, marehemu alionekana na majeraha mkononi na kichwani ambako alikuwa akivuja damu huku akilalamikia maumivu.
Baada ya hali ya marehemu kuwa mbaya katika Hospitali ya Rufani ya Mkoa, walimpa rufani ambapo alihamishiwa Hospitali ya Rufani ya Kanda ya Mbeya ambapo, alifariki dunia muda mfupi wakati akiendelea kupatiwa matibabu.
Kufuatia kifo cha kijana huyo, baadhi ya vijana wa Iyela waliamua kuandamana kupinga tukio hilo, wakidai kuwa linahusishwa na polisi, hivyo walianza kuwatafuta polisi wanaoishi eneo la kata hiyo na viongozi wa mtaa kwa nia ya kulipa kisasi.
Miongoni mwa viongozi waliokumbwa na kadhia hiyo ni Mwenyekiti wa Iyela II, Boaz Kyejo, ambaye alivunjiwa dirisha la nyumba yake wakimtuhumu kuhusika kuwaita polisi kwa ajili ya kufanya doria ya kuwakamata vijana wa kata hiyo baada ya kifo cha Mapunda.
Hata hivyo, Kyejo alisema hahusiki na tukio la kuwaita polisi wala doria na hata kifo cha kijana huyo hakuwa na taarifa nacho.
“Vijana wameharibu mali nyingi za mtaa huu, ikiwamo kuvunjwa kwa meza za soko na mali nyingine zilizokuwa sokoni hapo,” alisema Kyejo.
Kutokana na vurugu hizo, polisi wanadaiwa kuingilia kati kutumia nguvu ikiwamo kulipua mabomu.
Kwa upande wake mama mdogo wa marehemu, Justina Kilasa, alisema marehemu hakuwa na tabia mbaya, hivyo kitendo cha kukamatwa kwa madai ya kuhusika na uhalifu sio cha kweli, kutokana na marehemu kuwa na tabia njema.
“Mwanangu hakuwa mgomvi, alikuwa hajihusisha na tabia zozote mbaya, akitoka kwenye kibarua chake cha kuuza machungwa kule Sido anaenda ibadani na kurudi nyumbani,” alisema na kuongeza:
“Kwa kweli kifo hiki kimetushtua, mbaya zaidi Jeshi la Polisi limepiga mabomu ya machozi hapa msibani.”
Kilasa alisema kuwa mwili wa marehemu unahifadhiwa hospitali na wanasubiri kukabidhiwa kwa ajili ya maziko.
Mtendaji wa Kata ya Iyela, Anna Supalika, alisema amesikitishwa na uharibifu uliofanywa na vijana hao na kwamba hasara iliyopatikana haijabainika na kwamba shughuli za kiofisi zimesimama.
Alipoulizwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Mohammed Mpinga, alikiri kutokea kwa tukio hilo na kwamba taarifa rasmi ataitoa baada ya uchunguzi kukamilika.
Post A Comment: