WANANCHI wa vijiji 18 vya wilaya ya Iringa wamemilikishwa ardhi yao kisheria na kupata hati miliki za kimila za ardhi kupitia Mradi wa Urasimishaji Ardhi Vijijini (LTA).
Zoezi liliendeshwa na mpango wa kupunguza njaa na utapiamlo (Feed the Future) , ambapo naibu Mkurugenzi wa LTA , Malaki Msigwa , alisema jumla ya hati miliki za kimila 22,231 zimetolewa kwa wananchi wa vijiji hivyo miaka miwili iliyopita.
Msigwa alivitaja baadhi ya vijiji hivyo ni Kinywang’anga, Kiponzero, Magunga, Usengelindete, Ikungwe, Malagasi, Mgama, Ilandutwa, Lwato, Udumka, Mfukulembe, Muwimbi, Makoka na Isele.
Alisema jumla ya vipande vya ardhi 32,141 vilipimwa katika vijiji hivyo ambavyo ni kati ya vijiji 36 vinavyotarajiwa kunufaika na mradi huo unaotekelezwa kwa miaka minne tangu 2016 hadi 2019.
Alisema mradi wa urasimishaji ardhi unaofadhiliwa na Shirika la Misaada la Marekani (USAID) ambao ulikuwa na lengo la kuwawezesha wanavijiji kumilikishwa ardhi yao kisheria kwa kupanga matumizi bora ya ardhi ya vijijini pamoja na kutoa elimu ya sheria kuhusu haki za ardhi huku mipango bora ya ardhi ikiwa imeshaandaliwa kwa vijiji 29.
Pamoja na mradi kulenga kuvinufaisha vijiji 36 vya wilaya ya Iringa, Msigwa alisema kwa Jiji la Mbeya, vijiji vitano katika wilaya ya Mbeya vinatayarishiwa mipango ya matumizi bora ya ardhi na kila mwenye ardhi atapimiwa na kupewa hatimiliki ya kimila.
Alisema shirika hilo linafadhili mpango huo ili kuisaidia Tanzania kuwa na mfumo mzuri na wa wazi wa kulinda haki ya kumiliki ardhi kwa jinsia zote.
Alisema katika vijiji hivyo vya Iringa na Mbeya, zaidi ya hati miliki za kimila 70,000 zinatolewa kwa wananchi, hivyo kusaidia kupunguza eneo kubwa la ardhi ya Tanzania ambayo haijapimwa
Post A Comment: