VIONGOZI kadhaa wa chama cha ACT Wazalendo na wanachama wao wametangaza kukihama chama hicho na kujiunga na Chama Cha Mapinduzi (CCM) leo Ijumaa, Machi 2, 2018.
Akizungumza na wanahabari jijini Dar wakati wa kutoa maamuzi hayo, Katibu wa ACT Wazalendo Mkoa wa Dar es Salaam, Ernest Theonest Kalumuna, amesema yeye na Katibu wa ACT Jimbo la Ubungo na wanachama wao wengine wamefikia hatua hiyo kutokana na uongozi wa juu wa chama kushindwa kusimamia misingi thabiti ya chama chao.
“Tunautangazia umma hali mbaya ya chama chetu kilichoibuka kama chama mbadala wakati wa kuanzishwa kwake. Misingi ya chama haitekelezwi sawia, viongozi wetu wa juu wanapoungana na wanaohujumu juhudi za serikali kupigania wanyonge katika taifa letu.
“Hakuna tena kamati kuu, siku hizi kuna kikundi cha wapambe wachache wanakaa na kuamua mambo mazito ya chama, kujitoa kwenye uchaguzi bila mkutano halali, chama kimebaki kikundi cha wanaharakati tu, ofisi za majimbo zimefungwa zimebaki Mwanza na Kigoma wala viongozi hawashtuki.
“Tumeshtushwa na kauli za Kiongozi wa Chama Zitto Kabwe kuhamasisha Chadema wafanye maamuzi huku akisema sisi tunaunga mkono, anasema serikali hii ni rahisi zaidi kuiangusha. Hii ni ishara ya kwamba kiongozi wa chama amefilisika kisiasa.
“Atuambie ni Serikali ipi anataka kuiagusha? Ni ya Rais Magufuli ambaye Zitto alimsifia sana wakati akitoa hotuba yake ya kwanza bungeni Novemba 2015 baada ya kuingia madarakani au ni serikali nyingine? Mbona hasemi ni jambo gani ambalo Rais aliliahidi na hajalitekeleza?
“Hatuwezi kuendelea kuwa kwenye kikundi cha namna hii, kwa pamoja tunatangaza kujivua uanachama wa ACT Wazalendo na kujiunga Chama Cha Mapinduzi (CCM), hatuwezi kubaki kwenye chama kilichokosa mwelelekeo, kinaongozwa na kiranja anayetoa maagizo kutoka juu kwenda chini, bila kujali wanawapelekea akina nani. Tumeamua kwa nia moja kulitumia taifa kwa misingi ya utu na uzalendo,” alisema Kalumuna.
Post A Comment: