UMOJA wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) umesema viongozi wanaoshughulika na masuala ya sanaa na utamaduni wasiifanye kazi ya uhakimu kwa kufungia wasanii, akiwamo Roma Mkatoliki, kwa kuwa kunaweza kupoteza mapato na mabalozi wa nchi.

Akizungumza jana na wanachama wa umoja huo wilaya ya Dodoma mjini hapa, Mwenyekiti wa UVCCM, Kheri James alisema ameshuhudia baadhi ya kazi na wasanii wakifungiwa kutoshiriki sanaa kutokana na kwenda kinyume na sheria na taratibu.

Lakini akasema jambo hilo ni mambo madogo ambayo yanaweza kuzungumzika kabla ya kufikia hatua ya kuwafungia.

Alisema viongozi hao badala ya kufanya kazi ya uhakimu, ni vyema wakafanya kazi ya ualimu ya kufundisha watu namna ya "kuendana".

“Kuna wasanii ambao wameitangaza vizuri nchi yetu kimataifa na wamekuwa mabalozi wazuri, lakinipia wanalipa kodi kwa kazi zao za sanaa," alisema James, "sasa tunaweza kuwapoteza mabalozi na walipa kodi kwa makosa ambayo yanazungumzika bila kuhukumu.”

Mwenyekiti huyo alisema serikali ya CCM imeahidi ajira kwa vijana ambazo zinatokana na kuajiriwa na kujiajiri wenyewe, na kwamba kuna vijana wameamua kushiriki katika kazi za sanaa kwa kujiajiri.

“Sasa tusitumie kigezo cha sheria na taratibu kuwaangamiza watu ambao tungekuwa na uwezo wa kuwaelekeza na wangefanya vizuri zaidi," alisema zaidi mwenyekiti huyo.

"Niwaombe waliopewa dhamana ya kazi ya sanaa tuwe walimu walezi, uhakimu ufuate baadaye.”

Mwenyekiti huyo aliwaomba viongozi wa serikali  kuhakikisha mipango yao siyo kikwazo kwa watu wengine na kuwataka vijana wa chama hicho kutoa taarifa za viongozi wa serikali ambao ni kikwazo.

Alisema viongozi walioteuliwa si bora zaidi kuliko wengine bali watambue hiyo ni fursa ya kuwatumikia wengine.

Alisema endapo wataendelea kuwaacha vijana wakiangamizwa kwa kile kinachoitwa sheria na taratibu, hakuna atakayebakia.

“Mnasema mnataka kodi na wale ndio walikuwa wakichangia kodi kwa jasho lao mnawapoteza, hizi mbuga za wanyama zipo (viongozi) mnashindwa kutangaza leo kuna wasanii wanatoka kwenda kutangaza, tunawafungia kwa vitu vidogo.”

WAJIBU WAOAliwataka wabunge vijana kuangalia sheria zote zinazokandamiza watu na kuzifanyia marekebisho kupitia Bunge kwa kuwa ni wajibu wao na haiwezekani kutungwa sheria zinazowafanya watu kuwa watumwa kwa nchi yao.

“Kidonda tu kidogo kipo kwenye kidole wewe unakata mguu badala ya kukata kidole chenye kidonda," alisema James.

"Leo hii mmewakata kina Roma Mkatoliki... na wengine, mtu akinyanyuka nyie mnamrudisha halafu mtaimba nyie?“Wasanii wote mkiwafungia mtasimamia nini? Hii ni sawa na bwana shamba ambaye mashamba yote yatapimwa viwanja."

Wakati huo huo, Mwenyekiti wa UVCCM, Kheri James alisema vijana wa umoja huo wapo tayari kulinda heshima ya Tanzania kwa gharama yoyote dhidi ya vibaraka wanaotumika kuchafua taswira ya nchi kwa lengo la kuwanufaisha makaburu.

Alisema matumaini yaliyorejeshwa na Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais John Magufuli lazima yalindwe.

Alieleza kuanzia sasa endapo akiibuka mtu mwenye ujasiri wa kutukana, vijana hawatatukana bali watafanya litakaloonekana linafaa kwa maslahi ya taifa.

Alibainisha serikali imekuwa ikitenga mabilioni ya fedha kugharamia miradi ya maendeleo, lakini lipo kundi la watu linakejeli kuwa hakuna kinachofanyika.

Alisema watu wanasema hakuna demokrasia, lakini anayesema ni mbunge aliyechaguliwa kwa kura za wananchi.

Aliwataka vijana kuendelea kuhamasisha wananchi kujiunga na CCM kwani hakuna chama kinachotoa uhuru na demokrasia kwa watu wa kawaida kama CCM.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: