Naibu Katibu Mkuu wa Chadema (Bara), John Mnyika na Mwenyekiti wa chama hicho Kanda ya Serengeti, John Heche wameachiwa kwa dhamana baada ya kuhojiwa kwa zaidi ya saa mbili katika Kituo Kikuu cha Polisi jijini Dar es Salaam.

Mara baada ya kuachiwa, Heche ambaye ni mbunge wa Tarime Vijijini amesema kitendo cha viongozi wa Chadema kuripoti polisi na kukaa kwa saa tano bila kuhojiwa chochote na kutakiwa kuripoti siku nyingine ni sawa na kifungo cha nje.

“Hii ni mara ya tano ninaripoti polisi. Polisi Tanzania ni kama wametuhukumu kifungo cha nje, kila baada ya siku mbili wanataka turipoti kituo kikuu cha Polisi Dar es Salaam bila kujali unaishi wapi, gharama unazotumia kuja na kurudi Dar es Salaam na  majukumu yako mengine ya kikazi unayoshindwa kuyatekeleza. Kuna wakati inabidi kukataa uonevu huu,” amesema Heche 
 
Leo Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe; Katibu Mkuu, Dk Vicent Mashinji; naibu makatibu wakuu, John Mnyika (Bara) na Salum Mwalimu (Zanzibar) pamoja na Heche waliripoti kituoni hapo kwa ajili ya mahojiano.

Hata hivyo, mbunge huyo wa Tarime Vijijini na Mnyika waliendelea kuhojiwa huku wenzao wakiachiwa kwa dhamana, sababu ya wao kubaki kituoni hapo ikielezwa kuwa ni kitendo chao cha kutoripoti  Machi 16, 2018.

Mara baada ya kuachiwa viongozi hao wametakiwa kuripoti tena kituoni hapo Machi 27, 2018.

Heche amesema kitendo wanachofanyiwa si sahihi kwa maelezo kuwa baadhi yao ni wabunge na kwa sasa wanapaswa kushiriki vikao vya kamati za chombo hicho.

“Mimi napaswa kuwa katika vikao vya kamati za Bunge Dodoma. Mbali na hilo nikiwa jimboni kwangu, kutoka huko mpaka Dar es Salaam natumia nauli zaidi ya Sh1milioni. Hivi kwa nini hawalioni hili,” amehoji Heche.

Amesema kwa hali ilivyo ni vyema wakaelezwa hatima yao kwa maelezo kuwa mbali na kupoteza fedha, pia wanashindwa kushiriki shughuli za kibunge.

“Mfano wanataka turejee tena Jumanne ijayo (Machi 27, 2018). Hapa ninaondoka nakwenda Dodoma kushiriki vikao vya kamati, nitalazimika kuondoka jumatatu ili kuwahi. Sasa huu ni usumbufu kwa kweli. Katika hili sitakubali nitafanya kitu,” amesema Heche.

Wakili wa viongozi hao, Frederick kihwelo amesema Mnyika na Heche walizuiwa kuondoka na  kutakiwa kuandika maelezo.

"Baada ya kufika,  polisi waliwataka Heche na Mnyika ambao hawakufika Machi 16 . Walitaka wabaki baada ya wenzao kuondoka na kuwaagiza kuandika ahadi ya maandishi kuwa Jumanne ijayo watakuwepo,”amesema.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: