SERIKALI ya Ufaransa imeleta neema kwa vyuo vikuu nchini, baada ya kuingia makubaliano na Serikali kuvisaidia fedha za kufanya tafiti za kisayansi, pamoja na ufadhili wa wanafunzi kusoma Ufaransa.
Makubaliano hayo yalifanyika juzi jijini Dar es Salaam, ambao Tanzania iliwakilishwa na Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, William Tate Ole Nasha na Ufaransa ikiwakilishwa na Balozi wake, Frederic Clavier.
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya makubaliano hayo, Balozi wa Ufaransa Clavier alisema Ufaransa imefungua milango kwa vyuo vikuu Tanzania kushirikiana na vyuo vikuu vya Ufaransa.
Alisema elimu ni kipaumbele cha kwanza nchini Ufaransa, hivyo watamuunga mkono Rais John Magufuli katika kuhakikisha sekta ya elimu inakuwa mkombozi hususani nchi ikienda katika uchumi wa viwanda.
Alisema ushirikiano huo utawezesha wanafunzi wanaotaka kusoma shahada au shahada ya uzamili nchini Ufaransa kwa ufadhili maalum.
Kwa upande wake, Kaimu Mtendaji Mkuu wa Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (Costech), Dk. Amos Nungu alisema huwezi kuongelea utafiti bila ya kufanya utafiti.
Alisema makubaliano hayo ni fursa kwa Costech kujenga uwezo kwa wataalam nchini, kwa watu kwenda kusoma Ufaransa.
Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) - Tafiti, Prof. Cuthbert Kimambo alisema ushirikiano huo utasaidia kukuza utafiti na mitaala UDSM.
Alisema uhusuano utaimalika baina ya vyuo vikuu vya Tanzania na Ufaransa, pamoja na ushirikiano wa ngazi ya juu kiserikali.
Naye Mkuu wa idara ya lugha za kigeni na fasihi Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Dk. John Biseko alisema UDOM inatarajia kunufaika na ushirikiano huo hususani katika Nyanja ya tafiti pamoja na kupokea wataalam kutoka Ufaransa.
Naye Naibu Waziri Ole Nasha alisema ushirikiano huo utasaidia vyuo vikuu kupata misaada kutoka serikali ya Ufaransa.
“Ni ushirikiano ambao kila nchi itanufaika, vyuo vikuu nchini vitapata pesa kwa ajili ya kufanya tafiti, pia itafungua fursa kwa wanafunzi wetu wa vyuo vikuu kwenda kusoma nchini Ufaransa,” alisema Ole Nasha.
Ole Nasha alisema Ufaransa ni nchi yenye mfumo mzuri wa elimu, na elimu yake iko juu miongoni mwa nchi za Ulaya, Alisema uhusiano huo pia utasaidia wanafunzi wa shule za sekondari kufahamu lugha ya Kifaransa.
“Kwa sasa kuna shule nyingi zinazofundisha Kifaransa, lakini Serikali imeweka msukumo kuhakikisha lugha ya Kifaransa inafundishwa kwa kiasi kikubwa katika shule zetu,” alisema.
“Tunataka kujenga mazingira ya wanafunzi kuwa wanajifunza lugha ya kifaransa japokuwa somo la kifaransa ni rasmi katika mitaala yetu ya elimu, lakini tunataka kutoa msukumo mkubwa ili lifundishwe zaidi.”
Alisema mwanafunzi kujua lugha zaidi ya moja kutamsaidia kupata fursa katika ajira na kwamba kwa sasa kuna mtaala wa lugha ya Kifaransa katika shule za msingi
Post A Comment: