Kituo cha Redio Times cha jijini Dar es Salaam kimetakiwa kuwasilisha kipindi cha mahojiano waliyofanya na mwanamuziki Diamond Platinumz kwa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kwa ajili ya uchunguzi zaidi.
Mkurugenzi wa Times FM, Amani Misana amesema kuwa amepokea barua ya kuwataka wawasilishe kipindi hicho kilichorushwa Machi, 19, 2018 na kwamba leo wametekeleza agizo hilo.
“Tumepokea barua na tumefanya yale tuliyoagizwa ikiwamo kuwasilisha kipindi chote,” amesema kwa ufupi Misana.
Kaimu Meneja Mawasiliano wa TCRA, Semu Mwakyanjala amesema suala la kituo hicho kupewa barua ni la kiutawala zaidi na mamlaka hiyo haipo kwenye kitengo chake isipokuwa kama tayari barua imefika, wakati wa kutolewa uamuzi vyombo vya habari vitaalikwa.
Mwanamuziki Diamond alizua mjadala baada ya kuzungumzia suala la nyimbo za wasanii kufungiwa akimlalamikia Naibu Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Juliana Shonza kutowatendea haki wasanii.
Diamond hakuishia katika mahojiano hayo yaliyoongoza na mtangazaji Omary Tambwe, Machi 20 kupitia mtandao wa Twitter alimjibu naibu waziri huyo akisema ametumia njia hizo kumjibu kwa kuwa naye alitumia hizo hizo.
Hata hivyo, jana mamlaka za Serikali ikiwamo Baraza la Sanaa la Taifa (Basata) na Waziri wa wizara hiyo, Dk Harrison Mwakyembe walimshukia mwanamuziki huyo wakisema amefanya makosa kumshambulia naibu waziri kwa kuwa uamuzi anaotoa siyo wake binafsi.
Post A Comment: