Polisi mkoani Shinyanga wanamshikilia mzee mwenye umri wa miaka 90, Kachuka Malongo kwa tuhuma za kubaka wanafunzi watano wa Shule ya Msingi Tinde, Wilaya ya Shinyanga.

Akitoa taarifa kwa vyombo vya habari jana Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, ACP Simon Haule alisema kwamba wanafunzi hao walibakwa kwa nyakati tofauti na mtuhumiwa akiwarubuni kwa kuwapa pipi na pesa.

“Tumebaini chanzo cha tukio hilo kuwa ni tamaa na uchu wa mapenzi. Tayari tunamshikilia mtuhumiwa kwa mahojiano zaidi na uchunguzi ukikamilika tutampeleka mahakamani,” alisema Kamanda Haule.

Akizungumzia tukio hilo Kamanda Haule alisema kwamba mkazi wa Tinde, Amada Mganyizi ndiye aliyebaini kubakwa kwa wanafunzi hao Machi 21 saa 2:30 asubuhi. Hata hivyo, hakueleza kwa undani namna gani mkazi huyo alibaini kubakwa kwa watoto hao.

Alisema kwamba wanafunzi hao ambao majina yao yanahifadhiwa wana umri wa kati ya miaka minane na 12 na wanasoma katika shule za msingi Tinde A na B.

“Natoa rai kwa wananchi na wazazi kuwa makini na karibu na watoto wao ili kubaini mabadiliko yao. Lakini kitu kingine kikubwa, nawataka wachukue hatua za haraka wanapobaini watoto wamefanyiwa ukatili kama huu,” alisema Kamanda huyo.

Aliwaonya watu wazima wenye tabia hizo kuacha mara moja.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: