Serikali imetenga jumla ya shilingi Trilioni 1 mwaka wa fedha 2017/2018 kwa ajili ya kulipa madeni mbalimbali ya watoa huduma, wazabuni na watumishi wa Umma.
Mkurugenzi wa Idara ya Habari (MAELEZO,) Dkt. Hassan Abbasi ameeleza hayo leo Mjini Dodoma alipokuwa akiongea na waandishi wa habari juu ya utekelezaji wa miradi na ahadi mbalimbali za Serikali.
“Kati ya shilingi Trilioni 1 zilizotengwa kulipia madeni kwa mwaka huu wa fedha, shilingi Bilioni 896.3 zimeshalipwa kwa watoa huduma, wazabuni na watumishi wa Serikali,” alisema Dkt. Abbasi.
Amesema hesabu hiyo inajumuisha shilingi Bilioni 43 ambazo zimelipwa Februari, 2018 ikiwa ni malimbikizo ya wafanyakazi wa sekta ya Umma.
“Madeni mengine uhakiki unaendelea na yataendelea kulipwa siku zijazo na tutawajulisha,” alifafanua Dkt. Abbasi.
Vile vile amesema, Serikali katika kuwaondolea adha ya usafiri kwa wananchi wa maziwa makuu likiwemo Ziwa Nyasa, Tanganyika na Victoria. Kwa upande wa Ziwa Victoria, mkandarasi amepatikana na majadiliano ya mwisho na kusaini mkataba na kampuni ya STX ya Jamhuri ya Korea vitafanyika mwezi huu kwa ajili utengenezaji wa meli mpya itakayokuwa na uwezo wa kubeba abiria 1,200 na mizigo tani 400.
Kwa upande wa Ziwa Tanganyika zabuni kwa ajili ya utengenezaji wa meli mpya ya abiria na mizigo itatangazwa mwezi huu. Meli hiyo mpya itakuwa na uwezo wa kubeba abiria 600 na tani 400 za mizigo na italeta mapinduzi makubwa katika usafiri ziwani hilo.
Aidha Dkt. Abbasi amesema Julai mwaka huu nchi itapokea ndege kadhaa mpya ikiwemo Boeing Dreamliner na ukarabati wa viwanja vya ndege vya Kitaifa, Kimataifa na Kimkoa unaendelea kwa kasi kote nchini.
Post A Comment: