Nteghenjwa Hosseah, OR-TAMISEMI
Waziri wa Nchi OR-TAMISEMI Mhe. Selemani Jafo amekutana na Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi Pro. Makame Mbarawa na Naibu Waziri wa Ardhi Mhe. Angelina Mabula kujadili mustakabali wa mgogoro wa Ardhi uliopo kati ya wananchi wanaonzunguka eneo la uwanja wa Ndege wa Kia na mwendeshaji wa Uwanja huo Kampuni ya KADCO.
Mgogoro huo unaohusisha zaidi ya kaya 1200 zilizopo katika Mikoa ya Kilimanjaro na Arusha zinazotakiwa kupisha upanuzi wa uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro.
Kaya hizo ambazo zipo katika vijiji vilivyopimwa Kisheria lakini maeneo ya vijiji hivyo yanaingiliana na eneo la uwanja wa KIA hivyo kusabisha mgogoro baina ya Menejimenti ya Uwanja na wananchi wa maeneo hayo.
Hali hiyo ilipelekea kuundwa kwa timu ya Ufuatiliaji na utafutaji wa suluhu ya mgogoro huo ambayo inaundwa na wizara tatu za Tamisemi, Ujenzi Mawasiliano na Uchukuzi, Wizara ya ardhi, Wakuu wa Mikoa miwili ya Kilimanjaro na Arusha pamoja na wataalamu kutoka katika sekta mbalimbali za ardhi na mawasiliano ya anga.
Kupitia kikao hicho waliazimia kuwa vijiji hivyo vifanyiwe Uthamini upya ili wananchi wa maeneo hayo waweze kulipwa Fidia na kuachia maeneo hayo kwa ajili ya upanuzi wa kiwanja cha ndege.
Kwa Pamoja viongozi hao wamekubaliana kuanza mchakato wa kufuta hati za vijiji hivyo na kuanza kuwaelimisha wananchi juu ya umuhimu wa eneo hilo kwa maslahi mapana ya Taifa.
Mgogoro kati ya wananchi wanaozunguka uwanja wa ndege wa KIA na kampuni ya KADCO umekuwako toka mwaka 1998 na umesababisha misuguano na hisia kali kwa muda mrefu hali iliyosababisha Serikali kuamua kutafuta ufumbuzi wa kudumu wa mgogoro huu.
Post A Comment: