Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Profesa Simon Msanjila amekutana na wajumbe wa kamati ya maandalizi ya uzinduzi wa ukuta unaozunguka machimbo ya madini ya Tanzanite Mererani, Wilayani Simanjiro. Ukuta huo unatarajiwa kuzinduliwa na rais John Magufuli mapema mwezi Aprili.
Kikao hicho kilichoanyika jana Machi 18, 2018 kiliudhuriwa na Watumishi kutoka Wizara ya Madini, Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa na Makamanda kutoka Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ)
Akizungumza katika kikao hicho Prof. Msanjila amelipongeza Jeshi kwa ujenzi wa kasi wa ukuta huo na kuongeza kuwa ilikuwa ni kazi ya kujitolea na jeshi limeisimamia vizuri.
Kwa upande wake, Naibu Kamanda wa Oparesheni ya ujenzi wa ukuta huo, Luteni Kanali Rashidi Kanole amesema kuwa, siri ya ujenzi wa ukuta kuchukua muda mfupi tofauti na muda wa utekelezaji wake, pamoja na mambo mengine umetokana na kufanya kazi kwa kuzingatia utamaduni wa jeshi unaohusisha kiapo na uzalendo na kutafuta mbinu za changamoto bila kusubiri viongozi wa juu kwenda kutatua changamoto hizo.
Ujenzi wa ukuta huo ulipangwa kutekelezwa kwa kipindi cha miezi sita lakini umekamilika ndani ya kipindi cha miezi 3.
Sambamba na kikao hicho, pia, Prof. Msanjila amekutana na wadau wa madini wilayani humo kujadili masuala mbalimbali kuhusu biashara ya madini hayo mara baada ya ukuta wa kuzinduliwa.
Miongoni mwa yaliyojadiliwa ni pamoja na ulinzi shirikishi wa ukuta huo, biashara ya Tanzanite, uwazi wa biashara na suala la vitambulisho vya Taifa.
Kuhusu vitambulisho Prof. Msanjila amesema kuwa atakayeingia ndani ya ukuta huo ni yule tu atakayekuwa na kitambulisho cha Taifa.
Aidha, pande zote mbili Serikali na wadau wamekubaliana kukutana tena ili kujadili kwa kina suala la biashara ya madini hayo mara baada ya ukuta kuzinduliwa
Post A Comment: