Akiwa ametimiza siku 859 madarakani, Rais John Magufuli ametembelea nchi chache huenda kuliko watangulizi wake wanne.

Magufuli ametembelea Kenya, Uganda, Rwanda na Ethiopia katika kipindi chote cha utawala wake huku akitimiza miaka miwili, miezi minne na siku saba tangu aapishwe kuwa Rais wa Tanzania Novemba 5, 2015.

Huenda hilo lilimfanya jana atoe siri na sababu zinazomfanya asipende kusafiri mara kwa mara nje ya nchi.

Akiwa mjini Singida jana alikozindua kiwanda cha mafuta ya kupikia cha Mount Meru Millers Group, Rais Magufuli alisema amekataa zaidi ya mialiko 70 ya kwenda nje ya nchi kwa sababu hakuchaguliwa na Watanzania kwenda huko bali kuwatumikia.

“Nataka Tanzania yote niizungukie ndiyo maana sitaki kwenda nje, maana huko si kwenye jimbo langu, jimbo langu mimi ni Tanzania. Nimekataa mialiko zaidi ya 70. Niende nje kufanya nini wakati sijamaliza kutatua kero za wananchi.”

“Nataka nizitatue kero za wananchi walionipigia kura kwanza, walipanga foleni wakati wa mvua na jua kunichagua mimi na waheshimiwa wabunge,” alisema Rais Magufuli.

“Bado sijaenda, Iringa, Mbeya, Rukwa na sehemu nyingine, lazima nizunguke nchi yote kutatua kero za wananchi..” alisema.

Julai 4, mwaka jana, alisema alipata mialiko zaidi ya 60 kwenda nje ya nchi baada ya kuwa Rais, lakini aliikataa kwa sababu anataka kuishughulikia Tanzania kwanza, Alisema hayo akiwahutubia wakazi wa Sengerema katika uzinduzi wa mradi wa maji.

Alisisitiza kuwa hana haja ya kwenda nje ya nchi kwa sababu bado ana mzigo mkubwa wa kumaliza ufisadi. “Niende nje kufanya nini wakati nitaenda tu nikishastaafu, nataka nimalize kwanza haya ya hapa ndani,” alisema pia mwaka jana mjini Sengerema.

Alipozungumza na watendaji mbalimbali wa Serikali Ikulu jijini Dar es Salaam Novemba 7, 2015, Magufuli alifuta safari za nje kwa watendaji wote wa Serikali na kusisitiza kuwa kama kuna ulazima, mhusika atapaswa kupata kibali kutoka kwa Katiba Mkuu Kiongozi.

Baadaye akizindua bunge la 11, Novemba 20 mwaka 2015, Magufuli alisema kuanzia mwaka 2013 hadi 2015, safari za nje zilikuwa zimeigharimu Serikali Sh356.3 bilioni.

Ongezeko la kodi
Jana, Rais Magufuli katika uzinduzi huo wa kiwanda cha mafuta, aliagiza Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kupandisha kodi kwa waingizaji wa mafuta ghafi ya chakula kutoka nje ya nchi.

Alisema hatua hiyo itawezesha wawekezaji wa ndani wa viwanda vya mafuta ya chakula kupata soko, Rais Magufuli alitoa agizo hilo wakati ambao Serikali inafanya maandalizi kwa ajili ya bajeti ya mwaka wa fedha wa 2018/19.

Alisema anafahamu mchezo mchafu unaofanywa na waagizaji wa mafuta kutoka nje ya nchi ikiwa ni pamoja na kuua soko la ndani la mafuta ya chakula.

“Ninafahamu mchezo mchafu unaofanywa na waagizaji wa mafuta, wanapofanya hivyo lengo lao si kutengeneza soko la ajira bali ni kuua soko la mafuta,” alisema.

Rais Magufuli alisema, “wanachofanya wanaagiza mafuta kwa kisingizio kuwa ni crude oil (mafuta ghafi) yanayohesabika kama ni malighafi,” alisema.

Aliongeza kuwa, kwa kisingizio hicho, TRA na watu wengine hawawatozi kodi na wanapoyafikisha nchini waagizaji hao huyaweka kwenye madebe na kuyauza hivyo kutengeneza faida kubwa.

“Nataka mwaka huu... wabunge mko hapa na waziri uko hapa... na waziri wangu najua mnanisikia nataka mafuta hayo yanayoagizwa kutoka nje yatandikwe charge (gharama) kubwa sana,” aliagiza.

Alisema anafahamu waagizaji hao huwa wanajikusanya na kwenda bungeni kuzitembelea kamati za Bunge.

“Naomba wabunge na mawaziri msikubali lobbing (ushawishi) za namna hiyo, mnawaumiza wananchi,” alisema.

Rais Magufuli alisema mahitaji halisi ya mafuta ya chakula kwa mwaka ni tani 450,000 na nchi inazalisha tani 135,000 sawa na asilimia 30, huku asilimia 70 ya mafuta ikiagizwa kutoka nje.

Alisema wanapoagiza mafuta hayo wanatumia dola za Marekani, fedha ambazo zingeweza kutumika katika shughuli zingine.

Rais alisema mafuta ya chakula yanachukua nafasi ya pili ya bidhaa zinazoingizwa nchini kutoka nje.

“Lakini mtu wa kawaida angeweza kutuuliza kweli Tanzania tuna wajibu wa kuagiza mafuta, tutumie fedha yetu ya kigeni kununulia mafuta ya chakula?” alihoji.

“Mtu yeyote mwenye akili timamu atakushangaa, mimi ndugu zangu ni mtaalamu wa kutengeneza mafuta nimewahi kukaa viwandani ninafahamu mchezo mchafu wanaoucheza hawa waagizaji.”

Pia, alimuagiza Waziri wa Viwanda, Charles Mwijage akamweleze mwenzake wa Wizara ya Fedha, Dk Philip Mpango kuangalia namna wanavyoweza kuwapunguzia gharama za kodi wawekezaji wa viwanda vya ndani.

“Haiingii akilini kutoza Vat (Kodi ya Ongezeko la Thamani) na kutoza kodi zingine kwa mtu ambaye ana kiwanda hapa; anatumia umeme wa hapa, anatumia maji ya hapa, anatumia malighafi za hapa, ametengeneza mnyororo wa ajira mkubwa wa watu wa hapa,” alisema.

Aliongeza kuwa kiwanda kama hicho kitanunua umeme, hivyo Tanesco watachukua fedha na Wizara ya Maji pia itapeleka maji kwenye kiwanda.

“Yale maji yatalipiwa kodi na wakulima wataweza kuuza mazao yao na wafanyabiashara nao watapunguza gharama za kusafirisha bidhaa zao sababu kiwanda kipo karibu.”

Utekaji na mauaji
Akiwasalimia wananchi katika uzinduzi huo, Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk Mwigulu Nchemba alizungumzia utekaji na mauaji ya watu yanayoendelea nchini.

“Kasi hii unayoifanya na vitu vinaonekana ndio inayowasumbua wapinzani wa kisiasa, maana kama ni gari upepo umetoa matairi yote ndiyo maana ajenda za kisiasa zimekwisha,” alisema.

Dk Nchemba, ambaye ni mbunge wa Iramba Magharibi alisema kwa wale ambao ni adui wa Taifa na historia anayotaka kuiweka Rais wanapokosa ajenda huhamia kwenye zingine za kuchafua taswira ya Taifa.

“Kinachotafutwa katika mambo mengi yanayoonekana ni namna gani ya kuchafua taswira ya nchi yetu. Ndiyo maana yanapangwa maandamano,” alisema.

“Kinachotafutwa si kuwa na mabango, kinachotafutwa ni watu kukusanyika na ikitokea namna yoyote ya kutawanya watu, wafyatue risasi ili waseme Serikali imeua watu.

“Njama hiyo tumeiona na mimi nimemwelekeza IGP kwamba hata kupanga njama ya kuua ni kosa wachukue hatua kwa wale wanaopanga njama hizo na kuchafua taswira ya Taifa letu.”

Alisema kuna watu wanatumia mikusanyiko kwa lengo la kufanya mauaji ya watu ili kuichafua Serikali na kwamba, mifano ya maeneo ambayo matukio ya aina hiyo yalishatokea ipo.

“Mheshimiwa Rais ndio maana unaona vinyago vinyago vingi, kama hivi juzi ametokea kijana anasema ametekwa, eti ametekwa akapata na muda wa kutafuta pafyumu na nguo za kubadilisha ...utapata wapi muda wa kujiandaa,” alisema Dk Mwigulu.

Alisema ni vitu vya ajabu ambavyo watu wanatafuta namna ya kuichafua Serikali na jambo hilo sio la kucheza nalo.

“Hakuna sababu ya maandamano na hakuna sehemu ya kuandamania na wala hakuna ruhusa ya kuandamana,” alisisitiza.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: