Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya limeendelea kukabiliana na vitendo vya uhalifu ili kuhakikisha kuwa wakazi wa Mkoa huu wanaendelea kuwa salama na mali zao. 

Aidha Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya limeendelea na Oparesheni na Doria za mara kwa mara ili kudhibiti vitendo vya uhalifu pamoja na kuzuia matukio mbalimbali yakiwemo ya uporaji na ukabaji na kama mtakumbuka siku za karibuni kulijitokeza vikundi vya uhalifu vilivyojiita majina ya wakorea weusi, weupe. Hata hivyo kumekuwa na matukio mawili kama ifuatavyo:-

Watuhumiwa wa uhujumu miundombinu ya TANESCO
Mnamo 24.03.2018 majira ya saa 00.15 usiku askari Polisi waliokuwa katika doria na oparesheni ya kukamata wahalifu huko maeneo ya Mtaa wa Airport ya Zamani, Kata ya Iyela, Tarafa ya Iyunga, Jiji na Mkoa wa Mbeya na katika Doria hiyo walikamatwa vijana kumi na wawili akiwemo kijana mmoja ambaye alifahamika kwa jina la ALAIN ACHILE [22] Mkazi wa Airport ya zamani.

Mtuhumiwa huyu pamoja na wenzake baada ya kukamatwa walifikishwa kituo kikuu cha Polisi Mbeya Mjini na kufunguliwa mashitaka ya UZEMBE NA UKOROFI ambapo walishikiliwa na kuhojiwa.

Mnamo 25.03.2018 majira ya saa 10.45 asubuhi mtuhumiwa ALAIN ACHILEalidhaminiwa na ndugu zake na kwenda nyumbani kwao. Ilipofika majira ya saa 18.00 jioni zilipatikana taarifa kuwa mtuhumiwa huyo amefariki dunia.

Mara baada ya taarifa hizo, wananchi wa eneo hilo la Airport ya zamani hasa vijana walianza kufanya fujo kwa kutuhumu kuwa Polisi wamehusika na kifo hicho hivyo kwenda nyumbani kwa Mwenyekiti wa serikali ya Mtaa BOAZ KAZIMOTO [74] Mkazi wa Iyela kwa kumtuhumu kuwa yeye ndiye aliyewaita Polisi kwenda kumkamata marehemu ALAIN ACHILE na wenzake hivyo walipofika nyumbani kwa Mwenyekiti huyo walianza kuvunja madirisha ya nyumba yake, Baadaye walikwenda kwenye barabara za mtaa huo na kupanga mawe barabarani na kuchoma moto meza za wafanyabiashara wa Soko la Maendeleo.

Halikadhalika walikwenda Ofisi ya Afisa Mtendaji wa Kata ya Iyela na kubomoa milango yote, kuharibu samani za ofisi na kuharibu baadhi ya nyaraka mbalimbali za ofisi ambazo hadi sasa thamani yake haijajulikana. Sanjari na hayo pia walikwenda nyumbani kwa askari aitwaye H.4325 PC YOHANA wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia na kuvunja madirisha ya nyumba yake huku wakitoa kauli ya kuwa wataichoma moto nyumba hiyo.

Kutokana na vurugu hizo askari walifika eneo hilo ili kutuliza vurugu hizo lakini wakati wanafika wananchi hao walianza kurusha mawe ili kuwadhuru askari  waliokwenda eneo hilo.

Kutokana na vurugu hizo, Gari yenye namba za usajili PT 1987 aina ya Toyota Land Cruiser Mali ya Polisi Wilaya ya Mbeya mjini ilivunjwa kioo cha mbele kwa mawe hivyo kulazimu askari kufyatua mabomu ya machozi kutuliza ghasia hizo.

Aidha katika vurugu hizo watuhumiwa nane [08] wamekamatwa kuhusika na vurugu hizo ambao ni:-
  1.     ELIUD  DAUD [22] Mkazi wa Iyela
  2.     BARIKI MASUDI [30] Mkazi wa Iyela
  3.     FRANK  KILEMI [33] Mkazi wa Airport ya zamani
  4.     KRIST NELSON [33] Mkazi wa Airport ya zamani
  5.     ESTOM MBALO [24]  Mkazi wa Airport ya zamani
  6.     ROBERT MWANGUPILI [24] Mkazi wa Iyela
  7.     ISSA NELSON [26] Mkazi wa Iyela
  8.     FELIX MBILINYI [21] Mkazi wa Airport ya zamani.
Watuhumiwa hao wanahojiwa na Jeshi la Polisi na watafikishwa Mahakamani wakati wowote mara baada ya taratibu za kisheria zitakapokamilika. Aidha juhudi ya kuwasaka wengine waliohusika na kuanzisha vurugu hizo zinaendelea.

Nichukue nafasi hii kuwapa pole wazazi, ndugu na hata walioguswa na kifo cha kijana huyu, niwathibitishie wananchi kuwa Jeshi la Polisi halikuhusika na kifo cha kijana huyu kwa aina yoyote. Aidha nimefungua jalada la uchunguzi [PE] kupitia Ofisi ya Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai [RCO] ofisini kwangu kwa ajili ya uchunguzi wa kifo cha ALLAIN ACHILE.

KUKAMATWA KWA WATUHUMIWA WALIOINGILIA MIUNDOMBINU YA TANESCO.
Mnamo tarehe 23/03/2018 Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya kwa kushirikiana na maafisa wa Tanesco lilifanya Oparesheni katika maeneo ya vijiji vya Isebe na Isajilo vilivyopo Wilaya ya Rungwe kufuatia taarifa za siri toka kwa raia wema kuwa kuna watu wanaingilia miundombinu ya Tanesco katika vijiji hivyo pamoja na kufanya wizi wa nguzo za umeme na kuwaunganishia umeme wakazi wa maeneo hayo kinyume cha sheria.

Katika Oparesheni hiyo, watuhumiwa wanne [04] wamekamatwa kwa kosa la kuingilia miundombinu ya Shirika la Umeme [Tanesco]. Watuhumiwa waliokamatwa ni:-
  1.    IDD HAMIS MWAMBUSYE [31] Mkazi wa Bagamoyo.
  2.     BENARD KIBONDI [40] Mkazi wa Kikota
  3.     THOBIAS WILFRED [42] Mkazi wa Iponjola
  4.     Eng.GEOFREY MSUNGA [30] Mkazi wa Mbeya
Aidha miongoni mwa watuhumiwa hao baada ya kukamatwa na kupekuliwa majumbani kwao walikutwa na vifaa mbalimbali vya umeme ambavyo ni:-
  1.  Mita za umeme 27 aina ya Tropical
  2. Nyanya za umeme mkubwa na mdogo za aina mbalimbali
  3. Kitoboleo cha nguzo
  4.  Stay Insulator
  5.  Plaizi
  6.  Tester za umeme
  7.  Seal za mita za umeme
  8.  Vibao vya tahadhari vinavyobandikwa kwenye nguzo za umeme
  9.  Nguzo 57 za umeme ambazo walikuwa zikitumika kuwaunganishia umeme wananchi.
Watuhumiwa watafikishwa Mahakamani mara tu baada ya upelelezi kukamilika. Aidha msako mkali unaendelea kuwasaka watuhumiwa wengine wanaojihusisha na uhujumu wa miundombinu ya Shirika la Umeme – TANESCO katika maeneo mbalimbali.

WITO:
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya Naibu Kamishina wa Polisi MOHAMMED R. MPINGA anatoa wito kwa jamii kuacha vitendo vya kujichukulia sheria mkononi na badala yake wafuate taratibu za kisheria ikiwa ni pamoja na kutii sheria bila shuruti. 

Aidha anatoa wito kwa jamii kuachana na tamaa ya mali hasa kwa kujihusisha na vitendo vya kihalifu ili wapate mali na badala yake wafanye kazi halali.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: