Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe.william Ole Nasha ameitaka  ofisi ya Mkuu wa wilaya, Musoma, Polisi na Takukuru kuhakikisha ndani ya wiki mbili inafanya  uchunguzi wa namna fedha za  ujenzi wa Miundombinu ya  Shule ya Sekondari Kasoma zilivyotumika kwa kuwa kuna harufu ya ubadhirifu wa fedha hizo.

Naibu Waziri Ole Nasha ametoa agizo hilo  mkoani Mara baada ya kufanya ziara ya kukagua ujenzi na ukarabati wa Miundombinu ya Shule inayonengwa na Wizara hiyo kupitia programu ya Lipa kulingana na matokeo, (P4R).

Amesema fedha zinapotolewa zinalenga kuwaboreshea huduma wananchi hivyo amewataka wale wote wanaotumia vibaya fedha hizo kuacha kufanya hivyo.

Mheshimiwa Ole Nasha amekiri kuridhishwa na ujenzi uliofanyika katika baadhi ya shule za mkoa huo ambazo amezitembelea ikiwa ni pamoja na Shule ya Msingi Kamuguruki  na Shule Sekondari na  Nyasho.

Waziri Ole Nasha pia amewataka walimu  wote nchini kuhakikisha wanafuata maadili yao ya kazi pamoja na kuacha mara moja  kujihusisha na vitendo vya kimapenzi na wanafunzi.

Amesema kuwa wizara yake imepokea taarifa juu ya baadhi ya walimu kujihusisha kimapenzi na wanafunzi  jambo ambalo ni kinyume cha sheria za nchi pamoja na maadili ya utumishi wa umma.

Naibu Waziri huyo amesisitiza kuwa  serikali haitamvumilia mwalimu yeyote mwenye tabia kama hizo na kuongeza kuwa mwalimu atakayebainika kushiriki vitendo hivyo atashtakiwa kwa mujibu wa sheria za nchi.

Katika hatua nyingine Naibu Waziri  Ole Nasha ameahidi kutoa mabati Mia Tano kwa ajili ya  shule ya sekondari kiara na kujenga madarasa matatu katika shule  Msingi ya Kiara zilizoezuliwa kufuatia mvua kali iliyonyesha jana usiku na kufanya uharibifu wa madarasa mawili ya shule hiyo.

Pia Naibu Waziri Ole Nasha ametembelea chuo cha Maendeleo ya Wananchi Bweri
Kilichopo Wilayani Musoma mkoani Mara

Imetolewa na;
Kitengo cha Mawasiliano Serikalini,
WIZARA YA ELIMU,SAYANSI, NA TEKNOLOJIA.
2/2/2018
Share To:

msumbanews

Post A Comment: