MWILI wa mmiliki wa mabasi ya Super Sami, Samson Josiah, unadaiwa umekutwa na wavuvi mto Ndabaka eneo la Bunda – Lamadi akiwa amefariki dunia jana Jumatano, Machi 14,2018 jioni huku watu wa karibu na marehemu wakithibitisha kuwa mwili huo ni wake.
Machi 9, 2018 taarifa za kupotea kwa Josiah kwa zaidi ya wiki mbili zilianza kusambaa baada ya gari lake alilokuwa akitumia aina ya Toyota Land Cruiser kukutwa limechomwa moto katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti iliyoko mkoani Mara huku akiwa hajulikani alipo.
Msumbanews Blog imemtafuta Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara, Jafary Mohammed, ambaye amethibitisha kupokea taarifa hizo.
“Hata mimi nimesikia tu taarifa za kuokotwa kwa mwili wa Samson Josiah, sasa hivi ndiyo ninaelekea eneo la tukio ili kufahamu kilichojiri, kama ni yeye aliyeokotwa au ni mwingine. Lakini taarifa za kupotea kwake zilitufikia na tulizitoa kwa umma siku chache zilizopita, hivyo tuwe na subira, tutawaeleza baada ya kupata taarifa kamili,” alisema RPC.
Kwa mujibu wa familia ya Josiah, ambayo inaishi mkoani Mwanza, ilidai kuwa siku ya kupotea kwa kwake ambayo ni Februari 27, majira ya usiku, alimpigia simu mkewe na kumwambia kuwa atarudi nyumbani na mgeni, na hayo yakawa mawasiliano yao ya mwisho.
Mabasi ya Super Sami yanafanya safari zake kuanzia mkoa wa Mwanza, kwenda mikoa ya Dar es Salaam, Dodoma, Iringa na Kagera.
Post A Comment: