SERIKALI imesema haijazuia vyombo vya habari kukosoa utekelezaji wa sera, mikakati na programu zake na badala yake imewataka kuzingatia miiko na maadili ya taaluma hiyo yaliyoanishwa na sheria za kimataifa.

Hayo yamesemwa jana Jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi wa Idara ya Habari (MAELEZO) na Msemaji Mkuu wa Serikali, Dkt. Hassan Abbasi wakati wa uzinduzi wa Awamu ya 25 ya utafiti wa sauti ya wananchi iliyotolewa na taasisi ya Twaweza.

Dkt. Abbasi alisema kumekuwepo na mkanganyiko mkubwa kuhusu dhana  ya uhuru wa habari, hatua inayosababisha baadhi ya vyombo vya habari kuandika na kutangaza taarifa mbalimbali ambazo zimekuwa zikikiuka misingi ya sheria za nchi.

“Wapo baadhi ya watu wamekuwa wakifikiri dhana ya uhuru ni kusema chochote na kutumia lugha ya kejeli, hivyo ripoti hii ya utafiti tumeweza kuwa na wataalamu mbalimbali waliokuwa wakitoa mada na kujadili kwa kina misingi na miiko ya uhuru wa habari” alisema Dkt. Abbasi.

Alisema kuwa dhana ya uhuru wa habari ipo katika sheria mbalimbali za kimataifa iliyoanishwa katika misingi ya haki na wajibu, na hivyo ni wajibu wa wadau mbalimbali kuwawezesha wananchi na vyombo vya habari nchini kuweza kuelewa dhana hiyo.

Aliongeza kuwa Serikali imeendelea kuongeza wigo mpana wa uanzishaji wa vyombo vya habari nchini ikiwemo kutoa idadi kubwa ya leseni za uanzishaji wa vituo vya redio hususani katika maeneo ya vijijini, hatua inayolenga kuwawezesha wananchi kuweza kupata taarifa mbalimbali za umma.

Kuhusu taarifa ya utafiti huo, Dkt. Abbasi alisema Serikali itatumia taarifa ya ripoti ya utafiti huo kupata mrejesho na kuainisha maeneo yote ili kuchambua hoja na kuweza kuangalia maeneo yenye changamoto ili kuweza kuboresha mfumo wa utoaji na upatikanaji wa taarifa za Serikali kwa wananchi.

Kwa mujibu wa Dkt. Abbasi alisema Serikali tayari imetoa maelekezo kwa Maafisa Habari na Mawasiliano wa Taasisi zote za umma nchini kuweka utaratibu wa kutoa taarifa zake kwa umma kwa kuwa suala la utoaji wa taarifa si utashi na badala yake ni utekelezaji wa matakwa ya sheria.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Taasisi ya Twaweza, Aidan Eyakuze alisema katika utafiti huo uliohusisha jumla ya watu 1500, ulionyesha kuwa wananchi wana imani na taarifa na imani zinazotolewa na Viongozi Wakuu wa Serikali ikiwemo Rais ikifuatiwa na Waziri Mkuu.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: