Mkuu
wa Mkoa wa Manyara, Alexander Mnyeti akizungumza na wananchi wa kijiji
cha Narakauwo Wilayani Simanjiro juu ya mgogoro wa uongozi na kumuagiza
mkuu wa Wilaya hiyo mhandisi Zephania Chaula aitishe kikao cha
wanakijiji hao ili kujadili tatizo lao.
Mkuu
wa Mkoa wa Manyara, Alexander Mnyeti ambaye pia ni mjumbe wa kamati ya
siasa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwenye mkoa huo, akimkabidhi
aliyekuwa Mwenyekiti wa Kijiji cha Narakauwo, Saruni Ole Sanjiro kadi ya
CCM kati ya wananchi 3,500 wa Chadema waliojiunga na CCM jana.
WANACHAMA
3,500 wa Chadema katika Kijiji cha Narakauwo, Kata ya Loiborsiret
Wilayani Simanjiro, wamejiunga na CCM kwa lengo la kumuunga mkono Rais
John Magufuli na Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Alexander Mnyeti.
Wananchi
hao ambao awali walikuwa CCM, waliondoka kwenye chama hicho na kujiunga
na Chadema, baada ya kigogo mmoja kukata majina ya baadhi ya wagombea
waliokuwa wanawaunga mkono kwenye Kijiji hicho na kata hiyo mwaka 2015.
Akizungumza
jana wakati akiwapokea wanachama hao wapya kwenye mkutano uliofanyika
kijiji cha Narakauwo, Mnyeti ambaye pia ni Mjumbe wa kamati ya siasa ya
CCM Mkoani Manyara, alitoa onyo kwa wanasiasa wanaowayumbisha wananchi
wa eneo hilo.
Mnyeti
alisema kuna baadhi ya viongozi wa wilaya hiyo bado wamelala kwani
wanadhani huu ni wakati wa kufanya siasa ili hali ilishakwisha mwaka
2015 na huu ni wakati wa kufanya kazi. "Kuna
baadhi ya viongozi walikaa vikao usiku ili kukwamisha suala hili,
nawapa onyo la mwisho, kama kuna mtu anataka ubunge asubiri mwaka 2020
siyo leo," alisema Mnyeti.
Hata
hivyo, Mnyeti alimuagiza mkuu wa wilaya hiyo mhandisi Zephania Chaula
kuhakikisha anamaliza mgogoro wa uongozi wa kijiji hicho. "Mkuu
wa wilaya baada ya siku nne rudi hapa ufanye mkutano wa kijiji kama
hawa wajumbe wa serikali ya kijiji ndiyo tatizo fuateni taratibu zote
waondoke uchaguzi ufanyike upya," alisema Mnyeti.
Alimuagiza
mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya hiyo Yefred Myenzi
kuhakikisha uchaguzi mdogo wa kujaza nafasi za uenyekiti unaofanyia
Machi 25, ujumuishe na kijiji hicho.Katibu
wa CCM Wilaya ya Simanjiro, Ally Kidunda alisema eneo hilo halina
upinzani ila wanachama hao waliondoka kwa sababu ya hasira.
Kidunda aliahidi kutoa ushirikiano wa dhati kwa wanachama hao wapya ili kutimiza dhana ya CCM mpya na Tanzania mpya. Mmoja
kati ya wanachama hao wapya, Mathayo Lesenga alisema awali waliondoka
CCM baada ya wagombea waliokuwa wanawaunga mkono kukatwa majina yao.
Post A Comment: