Mmiliki wa mabasi ya Super Sami, Samson Josiah, ametoweka kwa zaidi ya wiki moja sasa na gari lake aina ya Toyota Landcruizer kukutwa likiwa limechomwa moto katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti mkoani Mara.
Gari hilo lililokuwa likitumiwa na mfanyabishara huyo ambaye ni mkazi wa Mwanza, lilikutwa katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti mkoani Mara jana likiwa limeteketea kwa moto.
Ofisa Habari wa Chama cha Wamiliki wa Mabasi (Taboa), Mustapher Mwalongo, amesema kuwa mfanyabishara huyo licha ya gari lake kukutwa limeteketea kwa moto, hawakukuta mabaki ya mwili wake.
"Gari lake limeteketea kweli lakini hatujabaini kama na yeye alikuwa kwenye gari lile kwa sababu waliofika eneo la tukio hawajakuta mwili au mabaki ya aina yoyote," alisema Mwalongo.
Alisema baada ya mmiliki huyo wa mabasi kutoweka tangu Machi mosi, kamati iliundwa ya kufuatilia sababu za kutoweka kwake na wapi alipo ambayo inashirikiana na familia.
"Kamati ilipopata taarifa kuwa kuna gari limeteketea kule Serengeti, walishirikiana na Jeshi la Polisi kwenda hadi eneo la tukio na kubaini kweli ni lake lakini ndani hawajabaini kama alikuwemo mle wakati linachomwa," alisema Mwalongo.
Alisema Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi huku kamati hiyo ikiendelea na jitihada mbalimbali za kumsaka na kwamba hakuna uthibitisho wa aina yoyote ya kuwa amefariki dunia akiwa ndani ya gari lililoungua.
"Hakuna taarifa rasmi za mfanyabishara huyo kufa licha ya baadhi ya mitandao ya kijamii kuandika kuwa amefariki dunia. Hakuna mwili uliokutwa katika eneo lile," alisema.
Alisema wawakilishi wa Taboa mkoani Mwanza wanafuatilia kwa karibu na kuwapa kila taarifa wanayoipata kuhusiana na tukio hilo.
Pia alisema hadi jana jioni kamati hiyo kwa kushiriana na askari wa wanyamapori walikuwa wanaendelea kumsaka mfanyabishara huyo katika hifadhi hiyo.
Kuhusu kutoweka kwake, Mwalongo alisema mara ya mwisho walikutana kwenye kikao cha kamati ndogo ya Taboa mkoani Mwanza Februari 26, mwaka huu.
Alisema kuanzia Machi mosi zilianza kuzuka taarifa za kutopatikana kupitia simu zake za mkononi hadi nyumbani kwake.
Mabasi ya Kampuni ya Super Sami yanafanya safari zake kati ya Mwanza na mikoa ya Dar es Salaam, Dodoma, Iringa na Kagera.
Post A Comment: