Tunda Sebastian.

DAR ES SALAAM: Kimenuka! Siku chache baada ya muuza nyago kwenye video za Kibongo, Tunda Sebastian kuonekana kimahaba akiwa na mtangazaji wa Kituo cha Clouds TV, Casto Dickson, mzazi mwenzake na mwanaume huyo ambaye pia ni Miss Arusha, Don Posh ameibuka na kutaka aachiwe baba watoto wake, Amani lina ‘full’ stori.

TUJIUNGE NA CHANZO
Kwa mujibu wa chanzo chetu makini ambacho kipo karibu na miss huyo wa mwaka 2016, kabla ya Tunda kuonekana kimahaba na Casto, miss huyo alikuwa tayari amezaa naye.

“Ukiangalia katika mitandao ya kijamii na hata kwa marafiki zake wa karibu, Posh alianza kuanika uhusiano na Casto kabla hata ya Tunda. Baadaye Casto akafunga safari hadi ukweni huko Arusha kutambulika kisha hatukukaa sana tukasikia ameshampa ujauzito,” kilisema chanzo hicho.

AMEZAA NAYE WATOTO MAPACHA
Chanzo kilizidi kutiririka kuwa, baada ya Casto kwenda kujitambulisha ukweni, miezi michache baadaye, Posh aliyewahi kutokea kwenye video kadhaa ikiwemo Hakuna Matata wa Billnass, alifanikiwa kujifungua watoto mapacha wa kike, Gianna na Giannca.

“Mapenzi yalianza kunoga hapo, Posh akawa akimposti sana Casto kisha akiambatanisha na ‘caption’ ya baba wawili na kuweka msisitizo wa kumtag kabisa jina lake,” kilimwaga ubuyu chanzo.

TUNDA AHARIBU
Wakati mapenzi ya Posh na Casto yakiwa angali hai, Tunda aliingilia kati ambapo picha mbalimbali zilianza kuzagaa zikiwaonesha maeneo tofautitofauti wakiwa katika mapozi ya kimahaba.

“Kuna picha nyingine zinamuonesha Tunda akiwa kwenye kioo huku nyuma yake akiwepo Casto tena wakishikana kimahaba kabisa na nyingine zikiwaonesha wakigusanisha vichwa vyao kimahaba yaani zipo nyingi tu,” kiliweka nukta chanzo hicho.

HUYU HAPA MISS ARUSHA
Baada ya chanzo hicho kumwaga ubuyu, Amani lilimtafuta Posh ambapo alipopatikana alikiri maelezo yote yaliyoelezwa na chanzo na kukazia kwa kueleza uhusiano wake na Casto.

“Siku ya kwanza nilivyoona picha hizo zikisambaa nilimuuliza Casto akasema ni picha tu na mimi nikaamini haraka kwa kuwa najua kabisa mume wangu hawezi kummiliki mwanamke yule, mara nyingine tena nikaona picha zikiwaonesha wakiwa Ukumbi wa Next Door, Masaki tena kimahaba nikashangaa sana.

“Ninachotaka sasa ni Tunda aniachie baba watoto wangu asitake kumfanya kama King Mswati sipendi. Atambue kuwa nimezaa naye mapacha kwa nini aingilie mapenzi yetu? Anajua tulipotoka?” alisema Posh.

Casto Dickson.

TUNDA ANASEMAJE?
Juzi Amani lilimtafuta Tunda bila mafanikio lakini hata hivyo, katika moja ya gazeti dada na hili la Risasi Jumamosi, Tunda alimzungumzia Casto kama mpenzi wake wa sasa huku akisisitiza kuwa ndiye atakayemzalia.

“Kwa sasa mtu wangu ni Casto na hayo maneno mengine sitaki kuyasikia kabisa jamani. Huyu ndiye ninayetarajia kuzaa naye. Nipo na maisha mengine kabisa kwa sasa.”

CASTO AMKATAA
Gazeti hili halikuishia hapo, lilimtafuta pia Casto ambapo alipopatikana alikiri kuzaa na Posh lakini akasema si mtu wake kwa sasa.

“Huyo kweli nilizaa naye lakini tumeshaachana. Si yeye tu, yupo Muna na pia yupo mwanamke mwingine nimezaa naye mtoto mmoja. Mbona wenziye wote hawa-complain (hawalalamiki), ananiona na Tunda ndiyo ana-complain? Kwanza huyohuyo Posh alikuwa akitaka kuolewa na bwana mwingine sijui, nikamwambia asubiri kwanza watoto wangu wafikishe mwaka ndiyo afanye anachokitaka. Kwa hiyo aniache na maisha yangu

“Kwanza hata kwenye mitandao ya kijamii ukiangalia katika akaunti zangu sijawafollow watu wote niliotoka nao kimapenzi au kuzaa nao zaidi ya watoto wangu tu,” alisema Casto.

TUWEKE REKODI SAWA
Casto kabla ya kukutana na Tunda, tayari ana watoto wanne aliowapata kwa mama tofauti. Amezaa mtoto mmoja na mfanyabiashara, Muna Love pamoja na Miss Arusha, Don Posh (watoto mapacha wenye umri wa miezi saba) huku pia akiwa na mtoto mwingine aliyezaa na mwanamke mwingine.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: