Mbunge wa Singida, Tundu Lissu amesema ameona taarifa ya Msemaji wa Ikulu, Gerson Msigwa, kwamba ndege aina Bombardier iliyokuwa imezuiliwa Canada inakuja nchini.

Kupitia ukurasa wake wa Instagram Lissu ameandika baadhi ya mambo ambayo angependa baadhi ya watu wanaodai kuwa alitumwa kipindi cha nyuma alipokuwa anazungumzia kushikiliwa kwa ndege hiyo Canada wafahamu.

 ==>>Hii ni kauli yake
Nimeona taarifa ya Msemaji wa Ikulu, Gerson Msigwa, kwamba Bombardier yetu iliyokuwa imezuiliwa Canada inakuja. .

Kufuatia taarifa hiyo, baadhi ya watu wamedai mitandaoni kwamba kuletwa kwa ndege hiyo ni pigo na aibu kwa mawakala wa mabwanyenye waliosababisha ndege yetu kushikiliwa Canada.

Mimi nauliza: Hivi 'mawakala wa mabwanyenye' waliosababisha ndege yetu ikamatwe Canada ni akina nani hasa??? .
Here are some basic facts: .

1) Mwaka 2003, kampuni ya Sterling Construction and Engineering Ltd. (SCEL), ilivunjiwa mkataba wake wa ujenzi wa Barabara ya Bagamoyo. Mkataba huo ulivunjwa na Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

2) Baada ya kuvunjwa kwa mkataba, SCEL ilishtaki Serikali ya Tanzania kwenye Mahakama ya Usuluhishi ya International Chamber of Commerce, London. Tunaambiwa baadhi ya hearings, au zote, zilifanyikia Dar Es Salaam. .

3) Mwezi December 2009 na baadae June 2010, Arbitral Tribunal ya ICC ilitoa uamuzi kwamba Serikali ya Tanzania ilivunja mkataba wa SCEL bila uhalali wowote na kuamuru Serikali kuilipa SCEL takriban USD milioni 25, na riba ya 8% kwa mwaka kuanzia tarehe ya hukumu hadi tarehe ya malipo ya mwisho. .

4) Kwa sababu tunazostahili kuambiwa , deni la SCEL halikulipwa kwa miaka saba hadi SCEL walipoenda kwenye Supreme Court of Quebec, Canada, na kupata amri ya mahakama kuikamata Bombardier .

5) Baada ya kusikia Bombardier imekamatwa, Waziri wa Mambo ya Nje, Dr. Augustine Mahiga, na Balozi wetu Canada, Jack Zoka, walitumwa kwenda Toronto kufanya mazungumzo na SCEL juu ya namna ya kujinasua na balaa hili. Waziri Mahiga na Balozi Zoka waliiomba SCEL isitoe habari za Bombardier kukamatwa hadharani. .

6) Tarehe 18 August, 2017, baada ya kupata nyaraka mbali mbali zinazohusu kukamatwa kwa Bombardier , nilitoa taarifa za kukamatwa ndege hiyo kwa waandishi wa habari Courtyard Hotel, Dar Es Salaam. .

7) Kesho yake tarehe 19 August, Kaimu Msemaji wa Serikali, Zamaradi Kawawa, alithibitisha kukamatwa kwa Bombardier  na kutulaumu sisi wapinzani kuwa ndio tuliosababisha ndege yetu ikamatwe Canada. .

8) Licha ya Serikali kukiri ukweli wa maneno yangu, tarehe 20 August, nilikamatwa na askari polisi walioniambia hawajui kosa langu ila wanatekeleza 'maagizo kutoka juu.' Nililazwa mahabusu Central Police Station hadi kesho yake nilipopelekwa kwa Mkemia Mkuu ili kupimwa mkojo. Nilipokataa kupimwa mkojo nilirudishwa mahabusu hadi kesho yake tarehe 22 August nilipoachiliwa huru bila kupelekwa mahakamani. .

9) Alfajiri ya tarehe 26 August, 2017, ofisi za kampuni ya Mawakili ya IMMA Advocates ya Dar Es Salaam, zilishambuliwa kwa mabomu na 'watu wasiojulikana.' Miaka ya nyuma, IMMA Advocates waliwahi kuwa mawakili wa SCEL. Hadi leo hakuna mtu aliyetuhumiwa au kukamatwa na kushtakiwa kwa kuhusika na shambulio hilo la kigaidi. Na hadi sasa Jeshi la Polisi halijatoa taarifa yoyote ya uchunguzi wa shambulio hilo.

10) Tarehe 7 September, 2017, siku kumi na moja baada ya shambulio la mabomu dhidi ya IMMA Advocates, ikawa zamu yangu kushambuliwa kwa risasi za submachine guns na 'watu wasiojulikana.' Nilijeruhiwa vibaya sana, lakini Mungu ni mwema sikufa. Hadi ninapoandika maneno haya, hakuna mtu hata mmoja aliyetuhumiwa au kukamatwa na kushtakiwa kwa kuhusika na shambulio hilo la kigaidi dhidi yangu. Na hadi sasa Jeshi la Polisi halijanihoji mimi wala dereva wangu kuhusiana na shambulio hilo na wala halijatoa taarifa yoyote ya uchunguzi wa shambulio hilo. .

11) Kwa kipindi chote tangu  alipovunja mkataba mwaka 2003 hadi tarehe 18 August, 2017, nilipozungumzia hadharani suala la kukamatwa kwa Bombardier Canada, Serikali ya Tanzania, haikuwahi kuwaambia Watanzania kwamba tunadaiwa mabilioni na SCEL kwa sababu ya kuvunja mkataba na baadae kushindwa kesi. .

12) Msemaji wa Ikulu, Gerson Msigwa, na kabla yake Msemaji wa Serikali, Abbas, hawajasema, hadi sasa, ni kwa nini Bombardier yetu ilikuwa imezuiliwa Canada. Hawajasema kama ni kweli au la kwamba ndege yetu ilikuwa imezuiliwa kwa sababu ya  kuvunja mkataba kimakosa .

13) Nafurahi kusikia taarifa za kuachiliwa kwa ndege yetu. Nitafurahi zaidi tukiambiwa Bombardier hiyo imeachiliwa kwa masharti gani, kwa vile tulikuwa tunadaiwa karibu USD milioni 40 zilizotokana na kuvunja mkataba na Serikali kushindwa kesi na SCEL.

Nawatakieni Pasaka njema.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: