Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI, Mhe. Selemani Jafo (Mb) akimkabidhi moja ya gari la wagonjwa aina ya Suzuki Maruti, Ashura Nkya ambaye ni Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Babati katika bandari ya Dar es Salaam jana.
Baadhi ya magari aina ya Suzuki Maruti ambayo Mhe. Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliamuru yagawiwe katika Mamlaka za Serikali za Mitaa ili kuhudumia Sekta ya Afya nchini.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(TAMISEMI), Selemani Jafo, ameendesha zoezi la kugawa magari 50 ya wagonjwa aina ya Suzuki Maruti (Ambulances) kwa Mamlaka za Serikali za Mitaa nchini Jijini Dar es Salaam.
Magari hayo ambayo awali Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliagiza yafanyiwe utaratibu wa kisheria wa kiforodha na yagawanywe kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa ili yatumike kwa kuwahudumia wananchi katika vituo mbalimbali vya afya nchini.
“Hii ni agenda ya Mhe. Rais ya kutaka kuhakikisha watanzania wanapata huduma bora, ambulance hizi ulaji wake wa mafuta ni mdogo sana na zitatusaidia katika halmashauri nyingi,”amesema Jafo.
Aidha, Mhe. Jafo amemshukuru sana Rais wa John Magufuli kwa kuonyesha mapenzi makubwa lakini pia amependezwa na Watumishi wa Wizara, Mikoa na Halmashauri zote kuweza kuhudhuria hafla hiyo muhimu iliyofanyika bandarini Jijini Dar es Salaam.
Naye Naibu Katibu Mkuu anayeshughulikia Afya Ofisi ya Rais TAMISEMI, Dkt. Zainabu Chaula amemshukuru Waziri wa Nchi TAMISEMI na Waheshimiwa Wabunge wote kwa utendaji wao na kuwataka wabunge kuwa na lugha ya ufahamu mmoja ili kuboresha utendaji Serikalini.
“Kwa niaba ya watendaji nawashukuru sana waheshimiwa Wabunge, nilitamani tutembee pamoja kwa maana ya kuwa na uelewa wa pamoja na ndio maana Mhe.Waziri amewakabidhi wabunge magari nao watukabidhi sisi,”Amesema
Charles Kichere Kamishna Mkuu wa Mapato Tanzania, amesema awali magari hayo aliyaona Mhe. Rais alipofanya ziara bandarini na kwamba magari hayo yalikuwa yameteleekezwa na mmiliki wake kutofahamika na ndipo rai, aliagiza kufuata utaratibu wa forodha na kuyataifisha magari hayo na kasha yagawiwe kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa nchini.
Kwa upande wake Mhe. Prof Norman Sigalla King, Mbunge wa Makete, amemshukuru Mhe. Rais kwa kutoa ambulance hizo kwa ajili ya kuimarisha huduma za mama wajawazito.
“kwanza nitoe shukrani za pekee kabisa kwa kupewa ambulance kwa ajili ya wilaya yangu ya Makete nakumbuka niliomba kwa ajili ya tarafa za Ukutama, Matamba, Magomba, Tulongwa na Niwaho”amesema.
Amebainisha umbali wa kata ya Ukutama hadi Makete mjini ni kilomita 70 na hivyo itawanusuru wakina mama dhidi ya vifo vya uzazi visivyotarajiwa.
Kaimu Mkurugenzi Halmashauri ya Wilaya Kigoma, Hakimu Ndatama amemshukuru Mhe. Rais kwa kuwapatia ambulance ambayo itaokoa vifo vya akina mama na watoto kwa kiasi kikubwa.
Post A Comment: