Ikiwa bado kuna vuguvugu la maandamano ya nchi nzima yanayohamasishwa kupitia mitandao ya kijamii, Tayari kumepangwa kufanyika kwa maandamano mengine makubwa ya amani ya kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli kwa utendaji kazi wake.

Maandamano hayo ambayo yanaratibiwa na kikundi kinachojiita Umoja wa Wakazi wa Jiji la Dar es salaam, kimesema kuwa maandamano hayo yanatarajiwa kufanyika tarehe 12 Aprili 2018 na kikundi hicho kimemuomba Rais Magufuli awe mgeni rasmi kwenye maandamano hayo kama atapata muda siku hiyo.

“Tumeona hakuna zawadi kubwa tutakayoweza kumpa Rais Magufuli zaidi ya kumuonesha kuwa tupo pamoja naye kwa kufanya maandamano ya hiyari, Maandamano haya tunategemea yatafanyika tarehe 12, Aprili 2018. Tunategemea yataanzia katika viwanja vya Karume na yataishia viwanja vya mnazi mmoja. Tunategemea ikiwezekana Mhe. Rais Magufuli awe mgeni rasmi,“amesema mratibu wa umoja huo, Charles Masele jana Machi 28, 2018 kwenye mkutano wao na waandishi wa habari.

Hata hivyo, Ndg. Masele amesema kuwa bado hawajarudishiwa majibu ya ombi lao kutoka kwa vyombo vya usalama na kama ombi hilo litakataliwa basi watafanya kongamano la kumpongeza Rais Magufuli badala ya maandamano.

Moja ya wajumbe  wa umoja huo waliyojitokeza kwenye mkutano huo, Athumani Kigora amesema kuwa Rais Magufuli amefanya mambo makubwa kwa kipindi hiki kifupi alichoongoza nchi hususani kwenye Afya, Miundombinu, Kudhibiti wala rushwa kitu ambacho yeye kama mtanzania lazima ampongeze.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: