Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limetangaza kuanza mchakato wa kutafuta kocha mpya wa timu ya taifa, ‘Taifa Stars’ baada ya mkataba wa kocha wa sasa Salum Mayanga kumalizika
Kaimu katibu mkuu wa TFF Kidao Wilfred, amesema lengo la kusaka kocha mpya ni kuleta changamoto mpya na kuitoa timu hiyo mahali ilipo kwenda hatua nyingine kwaajili ya mafanikio zaidi.
''Mchakato wa kuajiri kocha mpya utakuwa huru na anaweza kurudi Mayanga mwenyewe na tayari tumeshapokea maombi ya makocha wengi tu na tutatumia kamati ya watu waliobobea kwaajili ya kufanya mchujo wa majina hayo'', amesema.
Katika moja ya vigezo vitakavyozingatiwa ni ubora wa kocha pamoja na namna ambavyo shirikisho linaweza kumlipa kutokana na ubora wake. Aidha Kidao ameweka bayana kuwa wameshaongea na Mayanga kuwa yeye bado ni kocha pamoja na mkataba wake kuisha.
Taifa Stars chini ya Mayanga, jana imecheza mchezo wa kirafiki wa kalenda ya FIFA dhidi ya Algeria na kukubali kichapo cha mabao 4-1. Baada ya mchezo huo Stars itarejea nyumbani na kucheza na DR Congo Machi 27 kwenye uwanja wa taifa.
Post A Comment: