Kijana Allen Mapunda mkazi wa Kata ya Iyela anadaiwa amefariki jana Machi 25, 2018 saa chache baada ya kuachiwa kutoka Kituo Kikuu cha Polisi mkoani Mbeyaalipokuwa amekamatwa na jeshi hilo.

Taarifa za awali za tukio hilo zinaeleza Allen alikamatwa juzi akiwa na wenzake wakati wakicheza Pool Table na kupelekwa kituoni ambapo anadaiwa alidhoofika sana baada ya kupigwa na kuteswa na polisi ambao hatimaye walipoona hali yake imekuwa mbaya walimuachia huru jana mchana.

Baada ya ndugu kuona kijana wao yuko katika hali mbaya, walimkimbiza Hospitali ya Rufaa Mbeya ili kuokoa maisha yake lakini ilipofika jioni aliaga dunia.
Taarifa zinazidi kueleza kwamba, wananchi wa eneo hilo waliamua kupinga ukatili huo ndipo wakafunga barabara na kuchoma matairi,  vitendo vilivyopelekea Polisi kuwatawanya kwa mabomu ya machozi na kusababisha vurugu kubwa iliyodumu hadi saa tano usiku wa kuamkia leo.
Inadaiwa kuwa mwezi Januari, kijana mwingine kutoka Mtaa wa Airport (eneo jirani na Allen) alifariki saa chache baada ya kuachiwa kutoka Kituo cha Polisi huku ikidaiwa kuwa mauti hayo yalichochewa na kipigo kama cha Allen.

Global Publishers imemtafuta Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, SACP Mohammed Mpinga ili kuthibitisha na kutoa ufafanuzi kuhusu tukio hilo lakini simu yake imekuwa ikiita bila kupokelewa. Tutaendelea kuwajuza taarifa zaidi kuhusu tukio hilo.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: