Mkuu wa shule ya sekondari Kakonko katika Wilaya ya Kakonko mkoani Kigoma, Peter Rubonya amefariki dunia baada ya kujinyonga kwa kamba ofisini kwake.
Tukio hilo limetokea mapema leo Jumatatu Machi 26,2018 huku kukiwa na taarifa kuwa marehemu ameacha ujumbe unaosomeka "Mkurugenzi wa halmashauri ya Kakonko Lusubiro Mwakabibi asipothibitiwa ataua wengi"
Akielezea tukio hilo , mwalimu wa zamu Isaac Japhet amesema yeye alifika shuleni hapo mapema saa 12:30 kwa ajili ya kuwafundisha wanafunzi wa kidato cha nne masomo ya ziada baada ya kufunga shule wiki iliyopita, na baada ya kufika aligundua kuwa hana chaki ambapo mkuu huyo wa shule alimpatia chaki mlinzi ili awape wanafunzi.
Alisema baada ya muda mratibu elimu kata pamoja na mmoja wa wazazi walifika ofisini hapo wakiwa na shida na mkuu wa shule na baada ya kuelezwa kuwa yupo ndani ofisini waliamua kugonga mlango ili kuingia lakini hawakuweza kujibiwa na ndipo wakaamua kufungua mlango na kukuta mwili wa marehemu ukining’inia darini.
Mwalim Isaac ameaiambia Msumbanews blog kuwa marehemu ambaye alikuwa akifundisha pia masomo ya Kemia na Fizikia shuleni hapo hawakuwahi kusikia kuwa na mgogoro wowote wa kifamilia au kijamii, na kwamba mkewe ambaye ni mkufunzi katika chuo kikuu cha Dodoma UDOM alifika nyumbani kwake juzi akitokea Dodoma.
Naye mlinzi wa shule hiyo Kajoro Kajabojabo amesema alikutana na mkuu wa shule mapema asubuhi akiingia ofisini na kumuomba chaki ambazo alipewa na kuziwasilisha kwa walimu.
“Nilimuona kabisa tukasalimiana nikamuuliza kama ana weza kuwa na chaki, akaingia ofisini akanipatia boksi moja la chaki, nikachukua nikampelekea mwalimu aliyekuwa anahitaji ,alikuwa kwenye hali nzuri tu, lakini baada ya muda ndiyo tukio hilo likatokea”aMEsema Kajoro.
Mkuu wa wilaya ya Kakonko Kanali Hosea Ndagala akizungmza baada ya kutembelea shule hiyo na kumfariji mjane amesema polisi wanaendelea na uchunguzi wa tukio hilo ili kujua sababu ikiwa marehemu aliacha ujumbe wowote au lah.
Pia ametumia fursa hiyo kutoa wito kwa jamii kutokaa na mambo yanayowasonga na badala yake wayafikishe katika ngazi tofauti za serikali ,jamii au rafiki zao .
“Hatujajua sababu lakini ni muhimu jamii ikajenga utamaduni wa kueleza matatizo ya ndani yanayoyasibu , hii inasaidia sana kupunguza msongo wa mawazo na kuepusha madhara kama haya”,amesema.
Kamanda wa polisi mkoa wa Kigoma Martin Otieno amesema baada ya kupekuliwa kwa mwili wa marehemu huyo walikuta karatasi imeandikwa ujumbe kuwa Mkurugenzi wa halmashauri ya Kakonko Lusubiro Mwakabibi asipothibitiwa ataua wengi
Post A Comment: