Mbunge wa Nzega (CCM), Hussein Bashe amewahakikishia wananchi wa Tanzania kuwa hoja yake aliyoiwakilisha kwa Katibu wa Bunge kuwa haiwezi kukwamishwa na jambo lolote kwa madai hakuna kisichojulikana kinachoendelea kutoka katika nchi
Bashe ametoa kauli hiyo leo (Machi 08, 2018) wakati alipokuwa anazungumza na waandishi wa habari Jijini Dar es Salaam kwa lengo la kuelezea sababu zilizompelekea yeye kama Mbunge kuandika barua ya kutaka kuundwe kwa kamati ya uchunguzi dhidi ya matukio mbalimbali yanayoonesha kutishia umoja, usalama na mshikamano wa taifa la Tanzania.
"Madhumuni ya kikatiba ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ni kuwasemea wananchi, kuwatetea kwa hiyo natimiza wajibu wangu kama Mbunge sioni kama nitapoteza Ubunge wangu katika hili. Mimi ninaamini nitapoteza ubunge wangu kwasababu zifuatazo, endapo nitashindwa kutimiza wajibu wangu ndani ya Bunge, nikishindwa kutimiza wajibu wangu ndani ya Jimbo langu kwa maana nimeshindwa kuisimamia serikali katika kuleta maendeleo, nimeshindwa kutimiza ahadi wakati wa uchaguzi katika jimbo langu na mwisho wanaccm watakaposema kwenye mchakato wa kidemokrasia wa kura kwamba Hussein wewe hapana", amesema Bashe
ameendelea kusema
"Mimi ni muumini wa kiislamu ninaamini kila binadamu umauti utamfika (kifo) na chochote kitakachonifika ni kile ambacho amekipanga Mwenyezi Mungu lakini sina hofu yeyote kwasababu hili sio taifa la namna hiyo. Nikiwa kama Hussein sidhani hii hoja kama inakwenda kukwama kwasababu unapoikwamisha hoja unapaswa kusema unaikwamisha kwa kutumia misingi gani kama watu wanaamini kwa kila kinachotokea ndani ya ardhi ya Tanzania sioni kama itakwama".
Pamoja na hayo, Bashe ameendelea kwa kusema "Bunge limeshafanya maamuzi mbalimbali juu ya masuala mbalimbali katika rekodi ya nchi hii, kwa hiyo mimi nadhani ni muhimu tukatoa fursa jambo hili lifike Bungeni na likifika huko kama litakataliwa basi tujue ni kwasababu zipi na kama nilivyofanya kuwaambia watanzania ndivyo hivyo nitarudi kuwaambia limekataliwa kwasababu zipi na hapo tutajadili hatua za kufanya".
Kwa upande mwingine, Bashe amesema anasubiria majibu ya barua aliyotuma kutoka kwa Katibu wa Bunge Pamoja na Katibu Chama cha Mapinduzi (CCM) ambayo ameeleza dhamira na nia yake huku akisisitiza zaidi kuwa jambo hilo hajalifanya kwa mihemuko (kukurupuka) bali amefanya kwa umakini wa hali ya juu na utafiti wa kutosha.
Post A Comment: