Mashabiki wa DR Congo wameamsha sekeseke kwa shirikisho la soka nchini humo wakidai halikuwa na maandalizi mazuri na timu yao.

Hii inatokana na kero ya kipigo cha mabao 2-0 kutoka kwa Tanzania na hasa lile bao na nahodha, Mbwana Samatta.

Wengi wa mashabiki waliotoa maoni yao katika kipindi cha Okapi Radio wamelaani kitendo hicho,
Mtanzania Rashid Said anayeishi nchini Congo amesema wamekuwa wakilalamika sana na hasa bao la Samatta.

“Unajua huku hawaelewani sana na hasa maeneo, mfano hapa Lubumbashi na Kinshasa ni mbali sana na watu wana maisha tofauti utafikiri ni nchi mbili tofauti.

“Lakini linapofikia suala la mpira, wanaungana na wanazungumza lugha moja. Hawakupenda kufungwa na Tanzania lakini kufungwa na Samatta kumewaudhi zaidi.

“Wanalalamika sana na katika maoni yao wanataka hata viongozi wa shirikisho lao waachie ngazi,” alisema.

Samatta alifunga bao la kwanza katika mechi hiyo ya kirafiki kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, huku Shiza Kichuya akimalizia kazi kwa kufunga bao la pili.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: