Katibu wa chama cha ACT - Wazalendo Jimbo la Kigoma mjini, Azizi Ally ametoa onyo kali kwa madiwani wa chama hicho kuwa atakayekihama na kujiunga CCM atatengwa na jamii.

Kauli hiyo imetolewa leo Jumatatu Machi 5, 2018 mjini hapa kufuatia kuwepo taarifa ya madiwani wanne kupanga mikakati ya kukihama chama hicho na kujiunga CCM.

Ally amebainisha kuwa diwani yeyote atakayehamia CCM atakuwa amejimaliza kisiasa kwani jamii nzima ya watu wa Kigoma itamtenga na kamwe asitarajie kushinda tena udiwani katika kata yoyote.

"Tulifanya kazi kubwa kuhakikisha wanashinda udiwani mwaka 2015, tukatumia gharama kubwa ya fedha za kampeni na muda wetu. Kamwe chama hakitakuwa tayari kuona diwani wake akihamia CCM,"amesema Azizi.

Ili kuwadhibiti madiwani hao, amesema wote waliitwa katika kikao maalumu cha chama na kuhojiwa juu ya kuwepo taarifa ya kukisaliti chama chao na kujiunga CCM, jambo ambalo walikanusha.

"Tumekaa na wazee wa chama chetu na madiwani wote wamedai wapo tayari kupigania chama, isipokuwa mmoja ndio hakuwepo," amesema.

Kwa upande wake, katibu wa CCM Mkoa wa Kigoma, Naomi Kapambala ametamba kwamba kuna madiwani wa upinzani watajiunga na CCM wakati huu wa ziara ya katibu wa itikadi na uenezi wa CCM, Humphey Polepole.

ACT wana madiwani 19 katika Manispaa ya Kigoma Ujiji ambapo CCM ina madiwani wanane na Chadema mmoja.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: