Mabingwa watetezi wa ligi kuu soka Tanzania Bara Yanga SC wameibuka na ushindi wa mabao 2-0 ugenini dhidi ya Lipuli FC kwenye mchezo wa raundi ya 16 uliomalizika kwenye dimba la Samora Iringa
Yanga ambayo imepata ushindi kwenye mchezo wa tatu mfululizo ilianza kuonesha dalili za kushinda mapema baada ya kiungo wa kimataifa Papy Kabamba Tshishimbi kufunga bao la kuongoza dakika ya 19.
Bao hilo lilidumu hadi mapumziko kabla ya timu hizo kurejea dimbani na Yanga kupachika bao la pili kupitia kwa kiungo Pius Buswita dakika ya 56 na kuihakikishia Yanga kupanda kwenye msimamo hadi nafasi ya pili.
Yanga imefikisha alama 31 na kuizidi Azam FC yenye alama 30 hivyo itakaa katika nafasi ya pili ikisubiri matokeo ya mchezo wa baadae leo ambao Azam wataikaribisha Ndanda FC kwenye dimba la Azam Complex majira ya saa 1:00 usiku.
Katika mechi zingine za leo Singida United imeibuka na ushindi wa mabao 3-2 dhidi ya Mwadui FC. Singida United pia imesalia katika nafasi ya nne ikifikisha alama 30.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: