Naibu Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe. Juliana Shonza amewataka waandishi wa habari nchini kuzingatia maadili kwa kuandika habari zenye ukweli na uhakika kwa manufaa ya Taifa na Watanzania kwa ujumla.
Shonza ameyasema hayo leo katika maadhimisho ya siku ya Redio Duniani, ambapo kitaifa yamefanyika mkoani Dodoma na kuhudhuriwa na waandishi na watangazaji wa redio za jamii kutoka mikoa ya Arusha, Iringa, Morogoro, Mtwara, Shinyanga, Songwe, Geita, Mwanza, Kagera, Dodoma, Pemba, Unguja, Lindi na Songwe.
“Redio za jamii zimekuwa tegemeo kubwa la kupata habari kwa wananchi wa maeneo mbalimbali hapa nchini hasa pembezoni mwa nchi. Mwananchi haitaji kuwa na umeme anapotaka kusikiliza Redio,” alisema Shonza.
Amesema, ni vyema waandishi wawe wa kweli wanapotoa habari mbalimbali kwa wananchi ili kuepuka machafuko ya nchi kama ilivyotokea nchini Rwanda, ambapo chanzo cha machafuko hayo kilitokana na habari zilizotangazwa kupitia Redio.
“Wananchi wanategemea habari toka kwenu ili kujua namna Serikali inavyotekeleza majukumu yake pamoja na kutatua changamoto zao,” alisema Mhe. Shonza.
Vile vile kupitia Redio za Kijamii, wananchi ambao ni wakulima wanaweza kujua maeneo yalipo masoko kwa ajili ya mazao yao.
Naye, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dkt. Bilinith Mahenge amewataka waandishi wa habari kuitangaza Dodoma pamoja na fursa zilizomo mkoani humo kwa kuwa ni ya Serikali ni kuifanya Dodoma kuwa kituo cha mji wa kiuchumi.
“Mpaka sasa jumla ya watumishi 3000 wamehamia mkoani humu na kufikia Juni mwaka huu jumla ya watumishi wa Serikali 7000 watakuwa wamehamia. Hivyo fursa nyingi zitahamia mkoani humu,” alisema Dkt. Mahenge.
Post A Comment: