Watumishi wa Mahakama ya Tanzania Wilaya ya Kahama, mkoani Shinyanga, wametakiwa kuacha matumizi ya mitandao ya kijamii, hususani WhatsApp na Facebook wawapo kazini kwani inaathiri utendaji wa kazi.
Akizungumza na wafanyakazi hao mwishoni mwa wiki iliyopita , Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Kahama, Evodia Kyaruzi alisema mtumishi wa mahakama hatakiwi kujihusisha na hoja mbalimbali zisizokuwa na msingi katika mitandao ya kijamii.Kyaruzi alisema kujihusisha na hoja hizo, zikiwamo mambo ya kisiasa, siyo jambo jema “hasa kwa kazi hizi”, kwani inaweza kuchafua sifa ya watumishi wa mahakama.
Aidha, Hakimu Kyaruzi aliwataka watendaji wa mahakama za mwanzo na wilaya, Kahama kufanya kazi kwa uadilifu sambamba na kufuata sheria na maadili ya kazi, na kuacha kujihusisha na rushwa ambayo imekuwa ikipigiwa kelele kila kukicha.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Fadhili Mkurlu alisema baadhi ya mahakama nchini zimekuwa na uhaba wa mahakimu hali ambayo hufanya kesi nyingi zichelewe kuamuliwa.Alisema mfumo wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano(TEHAMA) utakapoanza rasmi katika mahakama wilayani Kahama, utasaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza mianya ya rushwa sambamba na kusaidia kupunguza gharama za karatasi ambazo zimekuwa zikitumika kwa wingi mahakamani.
Post A Comment: