Joseph Osmund Mbilinyi maarufu Sugu alizaliwa mnamo Mei Mosi, 1972 akiwa ni mtoto wa kwanza kati ya wanne upande wa maamyake, Desderia Lungu na baba anayeelezwa kuwa alikuwa mtumishi wa serikali.
Alianza elimu ya msingi mwaka 1981 katika Shule ya Msingi Sanawari iliyopo jijini Arusha na mwaka 1982 alihamia Shule ya Msingi Ligula mjini Mtwara.
Mwaka 1984 akiwa darasa la nne, alihama tena kutoka Mtwara hadi jijini Dar es Salaamalikojiunga na Shule ya Msingi Sokoine, wilayani Temeke.
Alihamia tena katika Shule ya Msingi Sisimba mkoani Mbeya ambako ndiko alikohitimu darasa la saba. Katika kitachake cha ‘Muziki na Maisha’, Sugu anaeleza kwamba sababu kubwa ya kuhamahama shule ilikuwa ni kuhamishwa kikazi kwa baba yake ambaye alikuwa mtumishi wa forodha.
Akiwa na umri wa miaka 38, Sugu aligombea ubunge wa Mbeya Mjini kupitia tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), akitumia kauli mbiu ya ‘Tumaini jipya kwa maendeleo ya wote’, akimaanisha yeye ni mwanga mpya wa maendeleo kwa wananchi wa jimbo hilo.
Safari ya kisiasa ya Mbilinyi ambaye ni msanii wa muziki wa Boongo fleva, hasa muziki wa hip hop aliyefahamika zaidi kwa jia la kisanii ‘Sugu’ au ‘Mr II’, ilianzia Juni 27, 2010 alipokabidhiwa rasmi kadi ya uanachama wa CHADEMA na Kaimu Katibu Mkuu na Mkurugenzi wa Mambo ya Nje ya chama hicho kwa wakati huo, john Mnyika.
Mbilinyi wakati akikabidhiwa kadi hiyo alikuwa na wasanii wenzake wa Bongo fleva, fred Malick ‘Mkoloni’ na Gerald Mwanjoka “G Solo’, tukio lililofanyika kwenye makao makuu ya CHADEMA yaliyopo mtaa wa Ufipa wilayani Kinondoni, jijini Dar es Salaam.
Sugu ambaye kwa wakati huo alikuwa anatokea nchini Marekani, siku mbili baadaye yani Juni 29, 2010 alitangaza rasmi kugombea ubunge katika Jimbo la Mbeya Mjini akipambana na aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo kwa tiketi ya CCM, Benson Mpesya.
Chini ya Kauli mbiu yake ‘Tumaini jipya kwa maendeleo ya wote’, Sugu alishinda uchaguzi huo uliofanyika Oktba 31, 2010 kwa kupata kura 46,411 dhidi ya kura 24,322 alizozipata mshindani wake, Mpesya wa CCM aliyekuwa akitetea jimbo hilo alilokuwa akiliongoza tangu mwaka 2000.
Baada ya kuupata ubunge Agosti 25, 2012, Sugu alianza harakati za kisiasa kwa kusafiri kwenda mji wa Houston katika Jimbo la Texas nchini Marekani ambako alikuwa mgeni rasmi kwenye hafla ya ufunguzi wa tawi la CHADEMA, ikiwamo kujadili mustakabali wa maendeleo ya Tanzania kwa ujumla wake.
Alirudi tena kwenye kinyang’anyiro cha uchaguzi wa 2015 ambako aliibuka mshindi kwa kupata kura 108,566 zikiwa ni kura nyingi kuliko mbunge yeyote katika majimbo yote ya uchaguzi nchini.
Anasema kwa muda mrefu katika maisha yake ya kimuziki pamoja na kuimba nyimbo za kuburudisha amekuwa zaidi mstari wa mbele kuimba nyimbo za kutetea haki za makundi mbalimbali katika jamii na Taifa.
Wakati akitangaza kugombea ubunge kwa mara yake ya kwanza, Sugu alisema umefika wakati wa kuhamisha jukwaa la mapambano ya kudai haki kutoka jukwaa la muziki mpaka la siasa kwa dhamira ileile ya kutumia kipaji chake cha kuimba na kukibadili kuhutubia kwa ajili ya kuleta mabadiliko nchini.
Post A Comment: