Wananchi wa wilaya ya Ulanga, Malinyi na Kilombero wameishukuru Serikali ya Awamu ya Tano kwa kutimiza ahadi waliyoitoa kwa wananchi hao ya kuwajengea daraja la mto kilombero ambalo lilikuwa kilio chao cha muda mrefu.

Wakizungumza mbele ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa katika kijiji cha Kivukoni, mkoani Morogoro, wakazi hao wamemueleza kuwa hivi sasa changamoto zao zimetatuliwa baada ya kukamilika kwa daraja hilo.

“Tunaishukuru Serikali kwa ujenzi wa daraja hili kwani limekuwa mkombozi kwetu wananchi wa wilaya za ulanga na kilombero kwani hapo nyuma vifo vingi vimetokea pasipo kutegemewa wakati tukitumia kivuko kufuata huduma za kijamii wilaya jirani ambapo ndio kuna huduma zote za muhimu”, amesema Bi. Zainabu Mtalanga

Aidha Waziri Prof. Mbarawa ametoa wito kwa wananchi hao kulilinda daraja hilo kwa kutojihusisha na vitendo vya kuchimba kokoto chini ya daraja, kuiba alama za barabarani na kuacha kupitisha mifugo juu ya daraja kwani Serikali imetumia gharama kubwa kujenga daraja hilo na barabara unganishi katika eneo hilo.

Ameongeza kwa sasa Serikali  ipo katika hatua za kujenga kituo cha polisi katika maeneo hayo ili kimarisha ulinzi na kuhakikisha usalama unakuwepo kwa saa 24 siku saba kwa wiki.

Naye Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS) mkoa wa Morogoro Mhandisi Dorothy Ntenga amemueleza Waziri Mbarawa kuwa ujenzi wa daraja hilo umejengwa kwa kuzingatia viwango vilivyowekwa kwenye mkataba na mkandarasi wa kampuni ya M/S China Railway 15 Group Corporation.

Kukamilika kwa ujenzi wa Daraja la Mto Kilombero umegharimu zaidi ya shilingi bilioni 50 ambazo zimegharamiwa na Serikali na daraja hilo litarahisisha shughuli za usafirishaji wa mazao, ufugaji na madini katika wilaya hizo na wilaya jirani.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: