WANAFUNZI wa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) kwa kushirikiana na madaktari bingwa chuoni hapo, wameanzisha tovuti maalum kusambaza uelewa wa masuala ya afya miongoni mwa jamii nchini.

Hatua hiyo, imetokana na ongezeko la maradhi sugu na vifo visivyo vya lazima vinavyotokana na jamii kukosa uelewa wa kutosha kuhusu namna ya kuzuia, kujikinga na kupata tiba ya magonjwa yanayoweza kutibika yakiwahiwa.

Akizungumza na Habarileo, kuhusu tovuti hiyo, mwanafunzi wa udaktari wa mwaka wa tatu chuoni hapo, Faith Castor alisema tovuti hiyo ya Daktari Mkononi imelenga kurahisisha utoaji wa elimu juu ya afya kwa ujumla katika jamii. “Unaweza kupata elimu sahihi juu ya magonjwa mbalimbali, visababishi vyake, dalili, jinsi ya kuyaepuka pamoja na elimu juu ya dawa.

Hii itasaidia jamii kuwa na uelewa zaidi juu ya magonjwa na kufika vituo vya afya na hospitali katika hatua za awali za ugonjwa,” alieleza. Alisema, upatikanaji wa matibabu mapema hupunguza kwa kiasi kikubwa madhara yanayoweza kusababishwa na ugonjwa. Alitolea mfano magonjwa yanayoweza kutibika mapema au kuzuia hatari kwa mgonjwa kama kuhara, malaria, Ukimwi, saratani na shinikizo la damu.

Kwa mujibu wa Kituo cha Kuzuia na Kusimamia Magonjwa (CDC) magonjwa yanayosababisha vifo nchini ni Ukimwi asilimia 17, malaria asilimia saba, maradhi ya kuhara asilimia sita, saratani asilimia tano, magonjwa ya moyo asilimia tatu, kifua kikuu asilimia tano na maambukizi ya kupumua asilimia 11. “Katika mafunzo yetu chuoni tumeshuhudia wagonjwa wengi wakija hospitali, tayari wakiwa katika hali ya hatari na wakati mwingine hawatibiki kutokana na kuchelewa kufika kwenye tiba kwa kukosa uelewa wa kutosha juu ya dalili za magonjwa,” alisema.

Alisema pia wamebaini jamii haipendi kupima afya hospitali na badala yake mtu anaposijikia vibaya, kutapika, homa au kuhara huenda kwenye duka la dawa na kununua dawa moja kwa moja kwa kisingizio cha malaria au UT I. John Manda, mwanafunzi wa mwaka wa nne, alisema kitendo cha kutozingatia upimaji wa afya ni hatari kwani wananchi wengi hujikuta wakiathirika na dawa wanazotumia kiholela au kupoteza maisha kwa kula dawa zisizo sahihi.

Alisema tovuti ya Daktari Mkononi inatoa elimu katika nyanja tofauti kama afya ya meno, afya ya mtoto, shinikizo la damu na magonjwa ya moyo, kisukari, magonjwa ya dharura, saratani, ujauzito na magonjwa ya wanawake na afya ya mazoezi. Elimu hiyo itatolewa bure katika tovuti ya www.daktarimkononi. com ambayo pia inatoa uwanja mpana wa maoni ya wananchi kuhusu masuala mbalimbali ya afya, yatakayojibiwa na wanafunzi hao kwa msaada wa walimu wao. Walimu na madaktari wanaohusika na kuchangia katika tovuti hiyo ni Dk Deogratous Mtei na Dk Julieth Joseph wote wa Muhas.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: