Wadau wa sheria, haki za binadamu na wafanyakazi wameeleza kusikitishwa na hatua ya mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kuwawajibisha hadharani watumishi wa umma.

Pia, wamebainisha kuwa mkuu huyo wa mkoa hana mamlaka ya kusimamisha shughuli za mabaraza ya ardhi ya kata kwa sababu yameundwa kisheria na utaratibu wa kuyaondoa lazima uwe wa kisheria.

Juzi, Makonda alipokea ripoti kutoka kwa wanasheria waliosikiliza kero za wananchi kwa uratibu wa ofisi yake.

Katika mkutano huo, Makonda aliwaita jukwaa kuu, wakuu wa idara ya ardhi na nyinginezo kutoka manispaa zote tano na kuwahoji kuhusu idadi ya migogoro na changamoto katika maeneo yao ya kazi.

Mkutano huo wa Makonda wa kutoa mrejesho kwa wananchi baada ya kupokea taarifa kutoka kwa wanasheria ulifanyika katika Ukumbi wa Diamond Jubilee na kurushwa moja kwa moja na kituo cha televisheni cha TBC 1 na redio ya TBC Taifa.

Mkuu huyo wa mkoa aliwahoji maswali mbalimbali maofisa waliokuwa wakiitwa mbele yake, ikiwa ni pamoja na kuwauliza ni vipi walipanda madaraja na kufikia wadhifa walionao.

Ni katika kuwahoji huko, mkuu wa idara ya ardhi Halmashauri ya Manispaa ya Ilala, Paul Mbembela alianguka na kupoteza fahamu.

Kutokana na Mbembela kushindwa kutoa idadi ya migogoro ya ardhi iliyopo, Makonda aliagiza apangiwe kazi nyingine na aondolewe katika nafasi yake ya sasa.

Hata hivyo, mkutano huo wa Makonda haujapita hivi hivi kwani kuna baadhi ya wanasheria na wadau wametoa mtazamo wao.

Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (Tucta), Tumaini Nyamhokya amesema hakupendezwa na kitendo cha mtumishi kuitwa na kuulizwa maswali ya kitakwimu huku akizomewa na watu.

Alisema walishaionya Serikali kuhusu kuwadhalilisha wafanyakazi hadharani kwa sababu ni kinyume cha utaratibu. Alisema kama kuna makosa yamefanyika basi uchunguzi ufanyike kisha hatua ichukuliwe.

“Tucta tutalitolea tamko suala hili ndani ya siku mbili zijazo. Haya mambo hayakubaliki, mtu anaweza kupata magonjwa ya kudumu kwa sababu ya jambo dogo tu,” alisema kiongozi huyo wa Tucta.

Akizungumzia suala la kuwajibishwa hadharani kwa watumishi wa umma, Felix Kibodya aliyewahi kuwa Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) alisema (watumishi) wana mamlaka za kinidhamu za kuwawajibisha.

Alisema Sheria ya Ajira na Uhusiano Kazini ya mwaka 2004 imebainisha hatua za kinidhamu dhidi ya watumishi ambao wanakiuka maadili ya kazi.

Alisema watumishi wana haki pia ya kusikilizwa kabla ya kuhukumiwa. “Haiwezekani jukwaani mtu akapewa adhabu palepale, vinginevyo utawala wa sheria hautakuwepo,” alisema Kibodya.

Alisema ipo mifumo rasmi ya kisheria ambayo inaruhusu mamlaka za kinidhamu kuchukua hatua.

Mratibu wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu (THRD), Onesmo Ole Ngurumwa alisema viongozi wanapaswa kuwa na maadili ya kuwawajibisha watu na kwamba jukumu hilo liko kwenye mamlaka ya kuajiri.

Ole Ngurumwa alisema mkuu wa mkoa alipaswa kuwasiliana na mkurugenzi wa halmashauri ili kumwadhibu mtu ambaye anadhani amekosea na si yeye mwenyewe jukwaani kuchukua hatua za kumwadhibu.

“Masuala ya kinidhamu yazingatie sheria ili kuepuka baadhi ya watu kuonewa. Mtumishi anatakiwa kupata muda wa kusikilizwa na kujitetea. Watumie mamlaka zinazoajiri ili zichukue hatua dhidi yao kama sheria inavyoelekeza,” alisema.

Mabaraza ya kata

Kuhusu kusimamishwa kwa mabaraza ya ardhi ya kata, Kibodya alisema yalianzishwa mwaka 1985 ili kushughulikia migogoro ya ardhi na halmashauri zilipewa jukumu la kuyasimamia.

Alisema mabaraza hayo yaliongezewa nguvu zaidi kwenye Sheria ya Ardhi ya Kijiji ya mwaka 1999 na Sheria ya Utatuzi wa Migogoro ya mwaka 2002, na mabaraza hayo yanasimamiwa moja kwa moja na Wizara ya Ardhi.

“Haiwezekani kesho mtu anakwenda kwenye Baraza la Kata anaambiwa mabaraza yamesimamishwa. Mambo ya kisheria hayawezi kuondolewa kwa matamko ya jukwaani,” alisema mwanasheria huyo.

Akizungumzia mabaraza hayo, Ole Ngurumwa alisema hizo ni taasisi ambazo zimeundwa kisheria na utaratibu wa kuzisimamisha ni lazima ufuate sheria hata kama watendaji wake hawatimizi wajibu wao.

Alisema wakuu wa mikoa na wilaya hawana jukumu katika mfumo wa utoaji haki na kwamba mahakama zinatakiwa kuwa huru bila kuingiliwa na mamlaka nyingine ya nje.

Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi la CUF, Julius Mtatiro katika andiko lake juzi alisema huenda Makonda ana nia njema ya kutatua matatizo ya watu wa Dar es Salaam. Hata hivyo, alisema matatizo na migogoro ya ardhi ni masuala mtambuka yaliyoshindwa ndani ya mfumo wa uendeshaji wa nchi.

“Matatizo hayo na migogoro ya ardhi ni tatizo la nchi nzima na kwa kweli njia ya utatuzi wake bado ni Mahakama na njia za kisheria,” alisema.

Mtatiro alisema, “Hakuna namna mkuu wa mkoa au wilaya au waziri akawa na mamlaka ya kutoa haki ya ardhi kwa mtu fulani aliyeonewa, hilo likitokea bado wasioridhika watakimbilia mahakamani. Kwa hiyo Mahakama hazikwepeki.”

Alisema amri ya mkuu wa mkoa ya kusimamisha shughuli za mabaraza ya ardhi ya kata mkoani Dar es Salaam inakiuka sheria na Katiba na haitatui matatizo ya ardhi yaliyopo.

Alisema mkuu wa mkoa angeweza kutumia nafasi yake na kuishauri Serikali ipeleke mabadiliko ya sheria mbalimbali bungeni ili kufuta mabaraza ya ardhi ya kata na kuweka vyombo vingine ambavyo vitaonekana ni kufanya kazi.

Mtatiro alisema migogoro ya ardhi maeneo ya mijini na vijijini ni tatizo la sheria, mifumo na taasisi zilizopo.

“Ili utatue matatizo hayo, unahitaji Katiba Mpya ambayo itajenga misingi thabiti ya utoaji haki kwenye sekta zote, ikiwemo ardhi,” alisema
Share To:

msumbanews

Post A Comment: