Wito umetolewa kwa wananchi wote kuanza kulipa Kodi ya Majengo ya mwaka 2017/18 mapema kwa kuwa ulipaji wa kodi hiyo umerahisishwa  ambapo wanaweza kulipa kwa kutumia njia ya kielektroniki.

Akizungumza jijini Dar es Salaam hivi karibuni Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Charles Kichere alisema hakuna muda utakao ongezwa ifikapo Juni 30, mwaka huu na badala yake faini itatozwa kwa kila mmiliki wa jengo atakayechelewa kulipa kodi hiyo.

“Kama mamlaka hatuoni sababu ya kuongeza muda wa kulipa Kodi ya Majengo ifikapo tarehe 30 Juni 2018 kwasababu tumewarahisishia wananchi ulipaji wa Kodi hii ambapo wanaweza kupata ankara ya malipo kwa majengo yaliyosajiliwa kwenye tovuti ya TRA au simu ya mkononi na kufanya malipo katika tawi lolote la Benki ya NMB au CRDB popote nchini au kwa njia ya mitandao ya simu ya Mpesa, Tigopesa au Halopesa”, alisema Kichere.

Kamishna Mkuu Kichere alisema kuwa, wananchi wafuatilie matangazo ya namna ya kulipa Kodi ya Majengo kwa njia ya kielektroniki katika mitandao ya kijamii na kwenye vyombo mbalimbali vya habari au wafike katika ofisi za TRA zilizo karibu na maeneo yao nchi nzima wapate utaratibu wa kulipa kodi hiyo kielektroniki.

Kichere aliongeza kuwa Kodi ya Majengo inalipwa kwa mujibu wa Sheria hivyo, ni muhimu wananchi walipe mapema kodi hiyo ili kuepuka usumbufu unaoweza kujitokeza mwishoni ikiwa ni pamoja na msongamano wa watu.

“Natoa wito kwa wananchi kwamba, wasisubiri mpaka mwisho ndio waanze kupanga foleni kwenye ofisi za TRA, wanatakiwa kulipa kuanzia sasa hivi katika ofisi zetu na wanaweza kulipa kwa kutumia njia ya kielektroniki kama nilivyoeleza hapo awali, kinyume na hapo itatubidi tutoze faini kwa atakayechelewa kulipa kodi hii ya majengo,” alisisitiza Kichere.

Kodi ya Majengo hulipwa kuanzia mwezi Julai mosi ya mwaka wa fedha husika hadi Juni 30 ya mwaka unaofuatia kwa kufuata Sheria, kanuni na taratibu,  hivyo, muda huu ni muafaka kwa wananchi kuanza kulipia kodi ya majengo mpaka ifikapo tarehe 30 Juni, 2018.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: