Na Ferdinand Shayo,Kilimanjaro
Maafisa Wanyamapori,  maliasili, ulinzi na uhifadhi wa mazingira katika hifadhi za taifa na mapori ya akiba ya wanyama ya serikali nchini waatanza kutumia teknolojia mpya ya kupambana na ujangili baada ya kubaini maeneo yaliyokithiri na ujangili na uharibifu wa mazingira  kwa kutumia simu na kompyuta ili kuimarisha doria na kudhibiti ujangili.

Maafisa hao walisema kuwa matumizi ya simu  na kompyuta zenye programu ya smart ambayo hutumiwa kuainisha maeneo hatarishi kwa ujangili na uvunaji holela wa miti yanaweza kuwekewa alama maalum za kitaalam na kuimarisha ulinzi zaidi.

Afisa wa chuo  cha usimamizi wa wanyamapori cha Mweka  Rudolf Philemon alisema kuwa matumizi ya teknolojia hiyo yatasaidia kukabiliana na kupunguza vitendo vya kijangili, uvunaji haramu wa misitu na kurahisisha mbinu za kuwakamata majangili.

Rudolf alisema kuwa kwa kutumia program hiyo ipasavyo inatarajia kupunguza vitendo vya ujangili katika Hifadhi za taifa na mapori ya akiba ili mali asili za taifa ziweze kuwa salama kwa manufaa ya Watanzania wote.

Mhifadhi wa pori la akiba la Ugalla mkoani Tabora  Braka Balagaye alisema programu hiyo pia itasaidia katika kukusanya ushahidi wa matukio mbali mbali ya majangili wanapokamatwa katika hifadhi za taifa, mapori ya akiba na misitu ya serikali ambao unaweza kutumika mahakamani.

“Programu hii itawarahisishia kazi askari wanaofanya doria katika hifadhi kuweza kuifanya doria yao kimkakati na kuzaa matunda kwa kudhibiti ujangili ambao ni tatizo sugu barani Afrika katika hifadhi nyingi” Alisema Baraka

Mkufunzi wa programu hiyo kutoka shirika la uhifadhi na ulinzi wa wanyamapori (WCS)  kutoka nchini Thailand Antony Lyman alisema, programu hiyo ikitumika ipasavyo ina uwezo mkubwa wa kutokomeza kabisa matukio ya ujangili katika hifadhi za taifa na mapori ya akiba.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: